Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

DKT. HOMERA AONGOZA  HUDUMA YA UFUATILIAJI WA HAKI MAGEREZANI

Imewekwa: 18 Sep, 2026
DKT. HOMERA AONGOZA  HUDUMA YA UFUATILIAJI WA HAKI MAGEREZANI

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, Septemba 17, 2026, ametembelea Gereza la Mahabusu Songea mkoani Ruvuma kwa ajili ya kufanya ufuatiliaji wa hali ya upatikanaji wa haki kwa Wafungwa na Mahabusu, pamoja na kusikiliza na kushughulikia changamoto zinazowakabili.

Akiwa ameambatana na timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi zinazoshughulikia masuala ya Haki Jinai, Mhe. Homera amesikiliza  changamoto zilizowasilishwa na Wafungwa na Mahabusu zinazohusu masuala ya Kisheria, zikiwemo ucheleweshwaji wa mashauri, upelelezi wa kesi na mashauri yaliyodumu kwa muda mrefu.

Mhe. Homera amesema jumla ya malalamiko 24 ya kisheria yatafanyiwa kazi  kupitia  taasisi za haki jinai ili  kuhakikisha mashauri yanashughulikiwa kwa wakati na haki inapatikana kwa makundi mbalimbali ya wananchi.

Katika ufuatiliaji huo, Waziri Homera  ameeleza  kuwa miongoni mwa kesi zinazochukua muda mrefu ni zile zinazohusu makosa ya mauaji na makosa ya uhujumu uchumi. Aidha, amesema idadi ya wafungwa na mahabusu katika Gereza la Mahabusu Songea imepungua kutoka takribani 300 hadi 152, kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na taasisi za haki jinai katika kushughulikia mashauri.

Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza la Mahabusu Songea, Murakibu Mwandamizi wa Magereza Robert Mabeja, amesema ziara hiyo imekuwa faraja kwa Wafungwa, Mahabusu pamoja na askari wa magereza, kwa kuwa imetoa fursa ya changamoto zao kusikilizwa na baadhi ya malalamiko  yao kujibiwa papo kwa papo, huku nyingine zikifikishwa katika taasisi zinazohusika kwa hatua zaidi.

Ziara ya Ufuatiliaji Haki Magerezani, iliambatana na Waziri  Homera kukabidhi  magodoro 30, pamoja na mchele na nyama kwa ajili ya Wafungwa na Mahabusu wa Gereza la  Songea.

Ufuatiliaji huo ni sehemu ya juhudi za Wizara ya Katiba na Sheria katika kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati kwa kila mwananchi, ikiwemo wafungwa na mahabusu, kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za haki jinai katika kushughulikia changamoto zinazochelewesha upatikanaji wa haki.