Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Elimu tuliyoipata itaondoa migogoro ya mirathi

Imewekwa: 27 Jul, 2023
Elimu tuliyoipata itaondoa migogoro ya mirathi

Na George Mwakyembe- WKS Nyasa

Wanakijiji wa kijiji cha Ngingama Kata ya Linga Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma wameshukuru Serikali kupitia Kampeni ya Mama Samia msaada wa kisheria kwa kuwapatia elimu juu ya mirathi ambayo imekuwa ikichangia kuleta migogoro ya ardhi katika jamii yao.

Akiongea kwenye mkutano uliofanyika tarehe 26 Julai, 2023 katika ofisi za kata ambapo watalaam kutoka Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na taasisi zingine za kisheria zilitoa mada mbalimbali kama vile mirathi, ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi Mwenyekiti wa kijiji hicho ndugu Raymond Kayombo amesema “elimu hii na iwe endelevu, binafsi sijawahi kupata elimu yeyote kuhusu kuandika wosia pamoja na namna ya kupata mirathi, na leo ni mara yangu ya kwanza tangu nizaliwe.”

Bw. Kayombo akaongeza “katika kijiji chetu cha Ngingama elimu hii tuliyoipata itapunguza migogoro ya ardhi hasa sisi tulioko huku kijijini kwasababu ardhi kubwa tuliyonayo tumerithi kutoka kwa baba zetu ambao wengi wao walishafariki na pia wazazi wetu hawakuandika wosia wowote.”

Naye Oigen Charles ambaye ni mkazi wa kijiji cha Ngimana amesema “fursa hii iwafikie na wengine, mimi nilikuwa sijui masuala ya haki za binadamu lakini leo nimepata elimu nzuri ambayo imekuwa funzo kwangu, binafsi elimu ya haki za binadamu pamoja na elimu ya mirathi sijawahi kuisikia popote, Tumekuwa tukishuhudia vitendo vya ukatili lakini hatukujua kama ni vya kikatili.”

Aidha, Bi Annamaria Charles ambaye ni mzee wa miaka zaidi ya 70 amesema “suala la wosia ni suala muhimu sana, unapofikia umri kama huu wa kwangu basi ni vyema ukaandika ili kuacha familia isiyo na migogoro.”

Vile vile Bi. Annamaria akaongeza “suala la mirathi hapa kijijni Ngingama limekuwa tatizo sana, lakini kwa elimu hii wananchi wameelewa vizuri, tunaiomba Serikali kuendelea kuwapatia elimu hii wananchi wengine hasa wa vijijini.”

Kampeni hii itafanyika katika kata zote ishirini za Wilaya ya Nyasa na inategemea kufikia tamati siku ya Jumatano tarehe 2 Agosti 2023.