Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

ELIMU YA HAKI  NA WAJIBU KUWAFIKIA WATUMISHI NA WANANCHI

Imewekwa: 09 Mar, 2026
ELIMU YA HAKI  NA WAJIBU KUWAFIKIA WATUMISHI NA WANANCHI

Serikali imejipanga kuimarisha utoaji  wa  elimu juu  ya haki  za  binadamu na wajibu  kwa  raia na watumishi wa Serikali kwa lengo la kujenga jamii yenye uelewa sahihi wa haki zake, uwajibikaji na ushiriki katika  maendeleo ya Taifa kupitia Katiba, sera, sheria  pamoja na mikakati ya kitaifa na kimataifa inayolenga kuhakikisha haki za wananchi zinalindwa na kuheshimiwa.

Hayo yamewekwa bayana na Naibu  Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Franklin  Rwezimula wakati wa ufunguzi wa kikao cha tathmini ya mahitaji ya elimu ya haki za binadamu na wajibu kilichofunguliwa  tarehe 5 Machi, 2026 katika ukumbi wa Hotel8 ya Morena jijini Dodoma. 

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Rwezimula alifafanua kuwa utoaji wa elimu hiyo ni muhimu kwa kuwa utasaidia  wananchi kutambua haki zao za msingi, kuzidai kwa njia halali na kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria za nchi. Vilevile, watumishi wa Serikali watajengewa uelewa katika masuala haya.

“Serikali imeendelea kuweka misingi imara juu ya uelewa wa haki za binadamu ili kujenga jamii inayoheshimu Sheria yenye uwajibikaji na inayoshiriki kikamilifu katika kulinda misingi ya haki za binadamu, utawaka bora, amani na mshikamano wa kitaifa." Amesema Dkt. Rwezimula. 

Katika hatua nyingine Naibu Katibu Mkuu amesema mwelekeo wa kuimarisha elimu ya haki za binadamu unaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo inasisitiza maendeleo jumuishi yanayozingatia utu wa binadamu, usawa wa fursa, utawala bora na uwajibikaji wa taasisi za umma. 

Kwa mujibu wa Dkt. Rwezimula, maendeleo ya kiuchumi hayawezi kutenganishwa na  ustawi wa wananchi, hivyo ni muhimu kuhakikisha makundi yote ya jamii yanapata elimu sahihi kuhusu haki na wajibu wao ili kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi. 

Rai imetolewa kwa washiriki wa kikao hicho kuweka mikakati madhubuti itakayohakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi katika makundi yote ya jamii zikiwemo asasi za kiarai,watumishi wa umma, taasisi za kijamii, sekta binafsi pamoja na makundi maalum kama wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu. 

Ushirikishwaji wa makundi mbalimbali katika utoaji wa elimu ya haki za binadamu utachangia kupunguza migogoro ya kijamii, kuimarisha uwajibikaji na kuongeza uelewa wa wanachi kuhusu ushiriki wao katika masuala ya  maendeleo na  ujenzi wa Taifa. 

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ibara ya 13 hadi 28 zinaainisha haki za msingi za binadamu ikiwemo usawa mbele ya sheria, haki ya kuishi, uhuru wa kutoa maoni, uhuru wa kujumuika na haki ya kufanya kazi na kumiliki mali.