Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Elimu ya sheria itumike kupunguza ukatili kwenye ndoa: Gekul

Imewekwa: 29 Jul, 2023
Elimu ya sheria itumike kupunguza ukatili kwenye ndoa: Gekul

Na William Mabusi – WKS Tunduru

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul (Mb) ametoa wito kwa jamii kutumia elimu ya sheria inayotolewa kwenye Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Sheria ya Mama Samia kupunguza na hatimaye kumaliza ugomvi kwenye familia zao na hivyo kuwa na jamii yenye amani ili kukuza maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Gekul ametoa wito huo wakati akihutubia wananchi wa vijiji vya Matemanga na Changarawe kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya ofisi ya Kata ya Matemanga Wilayani Tunduru, tarehe 28 Julai, 2023 ikiwa ni katika kutekeleza kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia.

“Tulikuwa hatujui haki zetu, watoto wa kike wamekuwa wakibaguliwa kwenye elimu na mirathi. Wanandoa wamekuwa wakipeana vipigo na wengine kuuana kitu ambacho ni kinyume na sheria, wananchi wanyonge wamenyimwa haki yao na hii ndiyo elimu tuliyokuja kuitoa kwamba mtu asinyang’anywe haki yake.” Alisema Bi. Gekul.

Mhe. Naibu Waziri amesema jamii ikifahamu sheria watoto wa kike watapewa haki sawa na watoto wa kiume, viboko vitapungua kwenye nyumba zetu kwani kwa mujibu wa sheria ya ndoa vipigo kwenye ndoa ni ukatili wa kijinsia, na hata kama wanandoa wakishindwana taratibu zipo za kuachana na namna ya kutunza watoto waliozaliwa katika ndoa hizo.

Aidha, Mhe. Gekul amewaonya vijana kutoingia kwenye ndoa bila maandalizi na kisha kuwatwika wazazi wao majukumu ya kuwalelea watoto watakaowazaa “ni wajibu wenu kisheria kuwatunza watoto wenu na siyo jukumu la bibi au babu zao, kama kijana wa kiume huwezi kutunza familia kama ambavyo sheria inakutaka subiri ujipe muda wa kujiandaa.”

Akitoa shukrani zake kwa Mhe. Waziri, Diwani wa Kata hiyo Mhe. Hamisi Kaesa alitoa ombi la kujengewa Mahakama ya Mwanzo kwani Mahakama iliyopo sasa imechakaa ombi ambalo Mhe. Naibu Waziri alikubali na kuwaahidi wanachi hao kuwa mwaka ujao wa fedha 2024/25 Wizara itapanga bajeti ya ujenzi wa Mahakama hiyo.