WANANCHI NJOMBE WAFIKIWA NA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA BILA MALIPO
Wizara ya Katiba na Sheria, imeanza kutoa Huduma za Msaada wa Kisheria kwa wananchi wa Mkoa wa Njombe, 18 Septemba, 2026 kwa Lengo la kuhakikisha wananchi wote wanapata haki kwa wakati na Usawa.
Akizungumza katika viwanja vya stendi ya zamani mjini Njombe, Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ambaye pia ni mratibu wa zoezi la utoaji wa huduma za kisheria Geofrey Mwachai alisema kuwa huduma hizi zinatolewa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria Awamu ya Pili lengo kuu ikiwa ni kuwafikia wananchi wote na kuhakikisha wanapata haki zao.
‘’Wananchi wengi hawafahamu wapi wanaweza kupata haki zao ama namna gani wanaweza kuzitunza, ila kupitia Kampeni hii ya Msaada wa Kisheria awamu ya pili tutatoa elimu ya kisheria katika maeneo mbalimbali ikiwemo elimu ya haki, wajibu na uraia, ndoa, mirathi, ukatili wa kijinsia na matunzo ya Watoto ili kuwawezesha wananchi kutambua haki zao na pia kufahamu nini wafanye pale wanapodhulumiwa haki hizo”alisema Wakili Mwachai.
Huduma zinatolewa katika viwanja vya stendi ya zamani Njombe ni pamoja na huduma za usuluhishi wa migogoro ya ardhi, ndoa, mirathi, matunzo ya watoto na masuala ya ukatili wa kijinsia, utoaji wa vyeti vya kuzaliwa, elimu ya masuala ya kisheria pamoja na uandaaji wa nyaraka za kisheria.
Wananchi wa Mkoa wa Njombe wanakaribishwa kufika katika viwanja vya stendi ya zamani ili kuweza kupata Huduma za Msaada wa Kisheria zinatolewa bure pasipo malipo ya aina yoyote na zitakazodumu kwa siku tatu, kuanzia leo 18-20 Septemba, 2026.