SERIKALI KUFANYIA MABORESHO TAASISI ZA HAKI JINAI
SERIKALI KUFANYIA MABORESHO TAASISI ZA HAKI JINAI
Serikali imekusudia kuzifanyia maboresho taasisi za Haki nchini ili kukabiliana na vitendo vyote vya uhalifu na kulinda Utu wa Mtanzania.
Hayo yamewekwa bayana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba 14, 2025 jjini Dodoma.
Rais Samia amesema kuwa, misingi ya mafanikio yote ya Nchi yanategemea Utawala wa Sheria ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Mahakama ya Tanzania ili Haki ipatikane kwa watu wote na kwa wakati.
"Tutaendelea kufanya mageuzi na maboresho katika taasisi zote zinazoshughulikia masuala ya Haki Jinai ili ziweze kukabiliana na vitendo vyote vya uhalifu."Alisema.
Maboresho hayo pia yamelenga katika kuuwezesha Mhimili wa Mahakama ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa majengo,vitendea kazi,watumishi,pamoja na kuimarisha matumizi ya TEHAMA ili kufanya kazi kwa ufanisi.
Ikumbukwe kuwa Rais Samia aliunda Tume ya Haki Jinai Nchini ili kuchunguza na kutoa mapendekezo ya kuboresha mfumo wa Haki Jinai ili kuhakikisha kuwa Sheria inatekelezwa kwa Haki na kwa njia inayoheshimu Haki za Binadamu.