Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

MWONGOZO WA TAASISI ZA HAKI JINAI KUBORESHA UPATIKANAJI HAKI

Imewekwa: 16 Sep, 2026
MWONGOZO WA TAASISI ZA HAKI JINAI KUBORESHA UPATIKANAJI HAKI

Wadau kutoka taasisi mbalimbali za haki jinai nchini wamekutana kwa lengo la kupitia na kuiboresha Rasimu ya Mwongozo wa Ufuatiliaji wa Majukumu ya taasisi hizo ili kuweza kuimarisha uwajibikaji na kuboresha upatikanaji wa haki kwa wananchi.

Akifungua rasmi kikao hicho leo, 15 Septemba, 2026 Mtumba jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, Balozi. Baraka Luvanda amesema kuwa lengo kuu la kikao hicho ni kupitia kwa kina rasimu iliyopo ili kubaini maeneo yenye mapungufu na kuyafanyia maboresho, ambapo msisitizo mkubwa utawekwa katika Viashiria Muhimu vya Utendaji (KPIs) ili kuufanya kuwa wa vitendo, unaopimika, na unaotekelezeka kwa tija.

“Viashiria vinavyoeleweka na kupimika vitasaidia kuimarisha uwajibikaji, jambo ambalo hatimaye litaboresha mfumo mzima wa haki jinai na kuharakisha upatikanaji wa haki kwa wananchi” alisema Balozi Luvanda.

Aidha, Balozi Luvanda aliongeza kuwa mwongozo huo unakusudia kujenga ushirikiano, kubadilishana uzoefu, na kusaidiana kutatua changamoto za kiutendaji ikiwa ni pamoja na kuondoa mazingira ya taasisi kulaumiana.

Awali, Mkurugenzi wa Katiba na Ufuatiliaji Haki, Wizara ya Katiba na Sheria, Jane Lyimo, akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu kufungua kikao hicho alitoa wito kwa wadau wote kushiriki kikamilifu ili kuhakikisha mwongozo utakaopatikana unakuwa na uhalisia na unatekelezeka kikamilifu.