Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. ULEGA AAHIDI USHIRIKIANO KUFIKIA MALENGO YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA

Imewekwa: 02 Oct, 2026
MHE. ULEGA AAHIDI USHIRIKIANO KUFIKIA MALENGO YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega, ameahidi kushirikiana kwa karibu na viongozi pamoja na watumishi ili kuhakikisha majukumu ya Wizara yanatekelezwa kwa ufanisi na hatimaye kufikia malengo na matarajio yaliowekwa na Serikali.

Mhe. Ulega ameyasema hayo leo, 1 Oktoba, 2026 Mtumba jijini Dodoma mara baada ya kuwasili na kukabidhiwa ofisi rasmi na aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo Mhe. Dkt. Juma Homera kufuatia mabadiliko yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 27 Septemba, 2026.  

Mhe. Ulega amesema yuko tayari kushirikiana na watumishi na viongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na kujifunza zaidi kuhusu majukumu na maeneo mbalimbali ya wizara na sekta ya sheria kwa ujumla ili kuweza kutekeleza majukumu kwa ufanisi.

“Mimi niko tayari kujifunza mambo mbalimbali kuhusu wizara hii na sekta ya Sheria kwa ujumla lakini pia kushirikiana na watumishi na viongozi ili kuhakikisha kazi zinafanyika kwa weledi na ubora na hatimaye kufikia malengo yaliyowekwa” alisema Mhe. Ulega.

Aidha, Mhe. Ulega  ametoa wito kwa watumishi wote wa wizara ya Katiba na Sheria kuhakikisha wanawajibika katika kutekeleza majukumu yao kwa wakati na kusisitiza kuwa hatarajii kuona hali yoyote ya uzembe kazini.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo tarehe 1 Oktoba, 2026 katika ofisi za wizara Mtumba Jijini Dodoma, na kushuhudiwa na viongozi wengine wa wizara akiwemo Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba, Katibu Mkuu Dkt. Seif Shekalaghe, Naibu Katibu Mkuu Balozi Baraka Luvanda pamoja na wakuu wa Idara na Vitengo vya wizara.