Huduma za Msaada wa Kisheria Zinapatikana Sabasaba Bila Malipo

Hyasinta Kissima – WKS Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini ametaka Wananchi wanaofika katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) kutembelea katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria ili kutapa huduma mbalimbali ikiwemo Msaada wa Kisheria.
Naibu Waziri Sagini ameyasema hayo Julai 5, 2024 jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea banda la Wizara kuangalia hali ya upatikanaji wa huduma hizo kwa Wananchi wanaotembelea banda hilo.
"Wapo Wananchi wanatoka katika maeneo mbalimbali Nchini na wengi kutokea jijini Dar es Salaam na wanahitaji msaada wa kisheria. Niwasihi sana kufika katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria na kupata huduma hizi bure. Wizara imejizatiti kuhakikisha kuwa kila Mwananchi atakayetembelea katika banda na mwenye shida atapata huduma. Wapo Mawakili wa Serikali, Wanasheria wenye weledi na ambao wapo tayari kuhakisha kuwa haki kwa kila Mtanzania inatendeka." Alisema Naibu Waziri Sagini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti, baadhi ya Wananchi waliofika katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria akiwemo Johnson Msemwa na Katarina Mpangilye wameonesha kufurahishwa na uwepo wa huduma hizo viwanjani hapo jambo ambalo limewawezesha kupata ushauri kuhusu masuala ya kisheria yaliyokuwa yakiwakabili.
“Nilikuwa nina changamoto kuhusu malezi ya watoto mara baada ya kutengana na mzazi mwenzangu. Nimefika katika banda hili la Katiba na Sheria nimepata elimu ya kutosha na Wataalamu wamenisaidia kufanya mawasiliano na mzazi mwenzangu na kupanga namna ya kuweza kufikisha huduma za matunzo kwa watoto.” Alisema mama mmoja ambaye hakupenda jina lake litajwe.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Ester Msambazi amesema kuwa mpaka sasa Kampeni hiyo imeshafika katika mikoa 7 na kufikia zaidi ya Wananchi 495,000 wakiwemo Wanawake, Wanaume na Watoto na wengi wamenufaika kwa kupata elimu, ushauri na utatuzi wa migogoro yao.
Wizara ya Katiba na Sheria katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara itaendelea kutoa huduma mbalimbali na kutatua changamoto mbalimbali za Wananchi ikiwemo migogoro ya Ardhi, Ndoa, Mirathi, ukatili wa kijinsia.