MATUMIZI YA TEHAMA SEKTA YA SHERIA KUCHOCHEA UTEKELEZAJI DIRA 2050
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, imeipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kuboresha utendaji wa Serikali, kuimarisha uwazi na uwajibikaji pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akiwasilisha pongezi hizo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati na Kamati kwa ujumla mara baada ya kupokea taarifa za utekelezaji wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST), pamoja na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), tarehe 22 Oktoba, 2026 jijini Dodoma, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Edwin Enosy Swalle amesema kuwa kuimarika kwa matumizi ya TEHAMA katika taasisi hizi kumeboresha zaidi ufanisi wa utoaji huduma.
Mhe. Swalle amesema kuboreshwa kwa matumizi ya Mfumo wa Usimamizi wa Mafunzo kwa Vitendo (LST-e-FIELD MIS 2026 ) na Mtaala wa Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (Legal Practice-Based Practical learning) ni hatua kubwa inayowasaidia wanafunzi kuwa bora zaidi pamoja na kupima kwa usahihi kile wanachojifunza.
Aidha Kamati hiyo imetoa wito kwa Mamlaka ya Usajili, Ufilisi na Udhamini RITA, kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoa elimu zaidi kwa wananchi juu ya matumizi ya mfumo wa e-RITA hasa katika eneo la kusajili ama kufanya mabadiliko ya vyeti vya kuzaliwa pamoja na kusajili Ndoa.
Awali, akiwasilisha taarifa za Utekelezaji wa Taasisi hizi, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega alisema kuwa Wizara na Taasisi zake zinaendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika kuboresha utoaji wa huduma, kuongeza uwazi na uwajibikaji pamoja na kuimarisha ufanisi wa utendaji kazi ili kuendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, inayotambua mapinduzi ya kidijitali kama nyenzo muhimu ya kujenga uchumi wa kisasa, shindani na jumuishi.
“Wizara na Taasisi zake zinaendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA. Hili linajidhihirisha kupitia mifumo ya kimkakati inayotumiwa na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo katika kusimamia mafunzo ya vitendo,” amesema Mhe. Ulega.
Mhe. Ulega aliwasilisha taarifa ya LST kuhusu hatua zilizochukuliwa katika utekelezaji wa Mfumo wa Usimamizi wa Mafunzo kwa Vitendo (LST-eFIELD MIS 2026), kiwango cha matumizi ya mfumo na matokeo yaliyopatikana katika kuboresha mafunzo ya vitendo na kuwaandaa wanafunzi kukidhi mahitaji ya soko la ajira pamoja na taarifa ya RITA iliyohusu hatua za kuboresha na kuimarisha huduma za usajili na uhifadhi wa kumbukumbu za matukio ya kijamii kupitia mfumo wa e-RITA kwa lengo la kuongeza ufanisi, kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, kuimarisha usalama na uaminifu wa taarifa pamoja na kudhibiti matumizi ya nyaraka zisizo halali.