Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

KAMATI YA BUNGE YA  UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YAPOKEA TAARIFA MBILI ZA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA

Imewekwa: 20 Oct, 2026
KAMATI YA BUNGE YA  UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YAPOKEA TAARIFA MBILI ZA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imepokea taarifa mbili za Wizara ya Katiba na Sheria kuhusu hatua za kulinda haki za watuhumiwa na marekebisho ya sheria 41 zilizobainika kukinzana, zilizowasilishwa na Waziri wa Katiba na  Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega, leo tarehe  20 Oktoba, 2026, katika ukumbi wa Frank Mfundo, Bungeni, jijini Dodoma.

Taarifa ya kwanza iliyowasilishwa  inahusu hatua zinazochukuliwa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (OTM), kwa kushirikiana na  taasisi nyingine zinazohusika na upelelezi, ukamataji na utaifishaji wa mali, kuhakikisha haki za watuhumiwa zinalindwa na mali zao zinatunzwa ipasavyo bila kupoteza thamani hadi mashauri yanayowahusu yanapohitimishwa mahakamani.

Taarifa ya pili inahusu hatua zilizochukuliwa katika kupitia na kufanya marekebisho ya sheria 41 zilizobainika kukinzana, ikiwemo kifungu cha 80(2) cha Sheria ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Sura ya 263, kwa lengo la kuondoa mkanganyiko wa kisheria na changamoto za tafsiri wakati wa utekelezaji wa sheria hizo.

Akiwasilisha taarifa hizo mbele ya Kamati hiyo, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Damas Daniel Ndumbaro (Mb), Waziri Ulega amesema Wizara ya Katiba na Sheria imejipanga kuimarisha utawala wa sheria, kulinda haki za binadamu na kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati.

Waziri Ulega amesema, hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa sheria zinazotungwa na kufanyiwa marekebisho nchini zinachochea maendeleo na ustawi wa wananchi. 
Aidha, taarifa hizo zinalenga kuimarisha ubora wa sheria kwa kuhakikisha kuwa zinakuwa na ulinganifu, zinaondoa migongano ya kisheria na kupunguza changamoto za tafsiri zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wake.

Wakizungumza katika nyakati tofauti tofauti Wajumbe wa Kamati hiyo wameshauri kuharakishwa kwa mapitio ya taarifa hizo na kufanya maboresho ya Sheria ikiwemo katika mashauri  yanayohusu mali ili kuhakikisha haki inatolewa kwa wakati na kulinda haki za wahusika ( Watuhumiwa).
 
Aidha, wameshauri  kuwekwa kwa muda maalumu wa kukamilisha uchunguzi wa mashauri hayo, kama ilivyo katika mashauri ya kibiashara, pamoja na kuendeleza  matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika kuhifadhi kumbukumbu sahihi za mashauri  na taarifa za watuhumiwa.