Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

TEHAMA KUONGEZA KASI YA UTENDAJI KWA MAENDELEO YA WANANCHI-DKT. HOMERA

Imewekwa: 25 Nov, 2025
TEHAMA KUONGEZA KASI YA UTENDAJI KWA MAENDELEO YA WANANCHI-DKT. HOMERA

‎Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera ametoa wito kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuongeza matumizi ya TEHAMA ili kuongeza kasi ya utendaji wa majukumu ya ofisi hiyo kwa lengo la kuhakikisha huduma bora zinatolewa sambamba na kusaidia kuwaletea wananchi maendeleo.

Dkt. Homera ameyasema hayo jijini Dodoma leo, Novemba 25, 2025 alipotembelea Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya Kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa lengo la kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Ofisi hizo sambamba na kufahamu mipango na mikakati ya kutekeleza majukumu yao.

“Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ina majukumu makubwa sana kwa kuwa mikataba yote ya serikali yenye thamani ya kuanzia bilioni moja inapitia hapa, hivyo ongezeko na kasi kubwa ya matumizi ya TEHAMA itawasaidia kujua ni kampuni gani yenye uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa ya serikali, kujua historia ya nyuma ya kampuni hiyo na kuhakikisha serikali haiingii hasara kwa kupitisha mikataba yenye lengo la kuwaletea wananchi maendeleo kwa maslahi ya nchi” amesisitiza Dkt. Homera.

 “Matumizi ya TEHAMA pia yatawasaidia kutekeleza shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na shughuli za kuuhabarisha umma juu ya majukumu yanayotekelezwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kasi iongezwe kwa mikataba yenye maslahi mapana zaidi ya Nchi, tuzingatie maelekezo ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassanya kuwa tunaenda kutekeleza miradi mingi kwa pesa za ndani, hivyo umakini zaidi unahitajika" aliongeza.

‎Kwa upande wake Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samwel Maneno aliweka bayana kuwa ofisi ni kiungo muhimu kwa mihimili mitatu ya serikali, ambapo ina wajibu wa kushauri katika masuala yote yanayohusu sheria.

Mhe. Dkt. Juma Homera ameambatana na Naibu Waziri Katiba na Sheria Mhe. Zainab Athuman Katimba na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Franklin Rwezimula.