Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

"Jamii Inahitaji Elimu Zaidi Kupinga Ukatili wa Kijinsia" Waziri Dkt. Pindi Chana

Imewekwa: 07 May, 2024
"Jamii Inahitaji Elimu Zaidi Kupinga Ukatili wa Kijinsia"  Waziri Dkt. Pindi Chana

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi amesema hayo  wakati  alipokutana na kufanya  mazungumzo na Wakili Onesmo Olengurumwa ambaye ni Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu - Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDC) kikao kilichofanyika Mei 7,2024 katika Ofisi za Bunge Jijini Dodoma .

Akizungumza katika kikao hicho kilichowahusisha Wataalamu kutoka ofisi hizo mbili, Waziri Chana amesema jitihada zaidi inahitajika katika kuongeza kasi ya utoaji wa  elimu kwa jamii ili kupinga matukio ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.

"Elimu ya ukatili wa kijinsia inapotolewa mapema kwa watoto huwasaidia kutambua haki zao na kuanza kuchukua hatua za kukabiliana na ukatili huo” alisema Mhe. Dkt. Chana

Katika kikao hicho, makubaliano mengine yaliyoafikiwa ni pamoja na kuwepo na mpango wa kuendelea na utoaji wa elimu kwenye vyombo mbalimbali vya habari juu ya athari za uvunjaji wa sheria, kupinga ukatili wa kijinsia ukienda sambamba na utoaji elimu kwa watoto wa shule za msingi  na kusisitiza kuwa Wizara yake itabainisha maeneo ambayo yanahitaji kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo THRDC katika kuendeleza jitihada za kutetea haki za binadamu.

Katika hatua nyingine kikao hicho pia kilijadiliana kuhusu  kukamilika kwa Mpango kazi wa Kitaifa wa Pili wa Haki za Binadamu, Ushiriki wa Serikali katika mifumo ya haki za binadamu ya Kikanda na Kimataifa ikiwa ni pamoja na kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa mikataba husika ambayo nchi imeridhia.