Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Jukumu la Wananchi Kupata Haki ni Lenu – Waziri Mkuu

Imewekwa: 22 Mar, 2024
Jukumu la Wananchi Kupata Haki ni Lenu – Waziri Mkuu

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) amesema Mawakili wa Serikali na Maafisa Sheria nchini ni jukumu lao kutoa haki kwa wananchi katika kuimarisha misingi ya haki na utawala bora.

Mhe. Majaliwa ametoa kauli hiyo alipokuwa anafungua Mkutano Mkuu wa siku tatu wa Mawakili wa Serikali tarehe 21 Machi, 2024 Jijini Dodoma.

”Serikali inaendela kuchukua hatua za maksudi na madhubuti kuboresha mfumo wa haki jinai, kujenga mazingira wezeshi kwa Mawakili wa Serikali na Maafisa wa Sheria ya kutoa huduma za kisheria kwa wananchi kote nchini, hivyo ni jukumu lenu kutoa haki kwa wananchi kwa wakati na pasipo kujali dini yake, rangi yake au itikadi ya siasa kwani kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watu wote ni sawa mbele ya sheria na wote wanapashwa kulindwa na kupata haki sawa,” amesema Mhe. Waziri Mkuu.

Akiongelea uhitaji wa huduma ya sheria amesema ”katika miaka ya hivi karibuni jamii imepitia mabadiliko na maendeleo mbalimbali katika maeneo ya kiuchumi, kiteknolojia, kiasiasa na kiutamaduni. Maendeleo hayo yameongeza uhitaji wa upatinakaji wa huduma za kisheria.”

Akihitimisha hotuba yake Mhe. Majaliwa amewaagiza Mawakili wa Serikali na Maafisa Sheria kutekeleze majukumu yao ya kisheria kwa uadilifu, weledi, uwajibikaji, uaminifu, usiri, umakini na kwa kujituma huku akiwata kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria katika kutekeleza kampeni ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia Lega Aid Campaign kwa kuipa uzito kama majukumu yao mengine ya kila siku.

Aidha, ameziagiza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Taasisi zingine za utoaji haki kufungua na kuimarisha ofisi katika ngazi za chini ili kuhakikisha huduma za kisheria zinawafikia wananchi wengi.

Awali akihutubia kwenye mkutano huo kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameyataja matunda ya kazi wanazofanya Mawakili wa Serikali akisema “katika miaka miwili ya kuwepo kwa Chama cha Mawakili tunashuhudia mchango mkubwa wa Mawakili wa Serikali katika sekta ya sheria ambao umewezesha ustawi wa masuala ya kiuchumi, kijamii, kisiasa, uwekezaji, utalii, uhusiano wa kimataifa, utoaji haki, utawala wa sheria, umoja wa kitaifa, na msaada wa kisheria, yote ni matunda ya uwepo wa Mawakili wa Serikali wenye ueledi na ufanisi katika kuchapa kazi.”

Akitaja mafanikio ya miaka mitatu ya Mhe. Rais hususan kwenye sekta ya sheria amesema ”miaka mitatu ya Dkt. Samia tumeona kuundwa kwa Tume ya Haki Jinai ambayo baada ya kazi yake imetoa mapendekezo ya namna ya kuboresha mfumo wa utoaji haki na sasa mapendekezo hayo yameanza kutekelezwa na ofisi nyingi za Serikali,” ameyataja mafanikio mengine kuwa ni kuendelea kutolewa kwa msaada wa kisheria kwa wananchi hasa wanyonge kupitia Kampeni ya Kitaifa ya Mama Samia Legal Aid Campaign, hivyo akatoa rai kwa wanasheria kutimiza wajibu wao wa kuwasikiliza watanzania, kwaelekeza na kuwasidia kupata huduma ya sheria na hapo watakuwa wameitendea haki Kauli mbiu ya mkutano huo inayosema  “Upatikanaji wa huduma za kisheria kwa Wananchi ni nguzo kwa ustawi wa jamii.”