Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Kabudi Mgeni Rasmi Mhadhara wa Kumbukumbu ya Benjamini Mkapa

Imewekwa: 02 Oct, 2024
Kabudi Mgeni Rasmi Mhadhara wa Kumbukumbu ya Benjamini Mkapa

Na Lusajo Mwakabuku - WyKS Dar

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi ameshiriki kama Mgeni Rasmi katika Mhadhara maalum wa Hayati Benjamini Mkapa, Rais wa Awamu ya Tatu ulioandaliwa na Chuo Kikuu Cavendish cha Uganda leo tarehe 01/10/2024 katika ukumbi wa hotel ya Johari Rotana Jijini Dar es salaam.

Akitoa salamu za ufunguzi katika mhadhara huo, Waziri Kabudi alisema kwake hii ni fursa adhimu kuhutubia mkutano huu unaosherehekea maisha ya kiongozi aliyekuwa na maadili na mchapakazi na kwamba kumbukumbu ya Benjamin Mkapa ina nafasi ya pekee katika mioyo ya wengi kwani inatuwezesha kutafakari juu ya uongozi na maono ya mtu ambaye maono yake yalivuka mipaka ya Tanzania.

“Tunaposherehekea urithi wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin William Mkapa, kiongozi ambaye ushawishi wake unaendelea kutengeneza maisha yetu ya sasa na yajayo, ahadi yake ya kuongoza kwa heshima, maono, na uwajibikaji kwa watu wake ni urithi ambao sote tunajitahidi kuudumisha. Urithi wake unaendelea kuishi katika mioyo ya wale aliowaongoza.” Alisema Kabudi.

Waziri Kabudi alieleza pia kuwa maisha ya Benjamin Mkapa ni mfano mzuri wa uongozi, diplomasia na uwezo wa maono. Alikuwa Rais wa tatu wa Tanzania na Chansela wa pili wa Chuo Kikuu cha Cavendish Uganda. Katika majukumu yote mawili, alifanya kazi bila kuchoka ili kuimarisha uhusiano ndani ya Afrika Mashariki na katika bara zima.

Aliendelea kusema kuwa Marehemu Mkapa alielewa umuhimu mkubwa wa utulivu wa kikanda, si tu kwa ajili ya ustawi wa mataifa binafsi bali kwa ajili ya kuendeleza elimu, ukuaji wa uchumi, na sekta binafsi katika Afrika iliyounganishwa.

Mhadhara huu ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Cavendish Uganda ni mhadhara watatu baada ya kufanyika mihadhara miwili ya awali iliyofanyika Novemba 2022 na 2023 Kampala, Uganda.