Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Kamati ya Bunge Yapokea Ufafanuzi wa Serikali Katika Marekebisho ya Sheria

Imewekwa: 23 Oct, 2023
Kamati ya Bunge Yapokea Ufafanuzi wa Serikali Katika Marekebisho ya Sheria

Na William Mabusi - WKS Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imepokea ufafanuzi wa Serikali wa baadhi ya vifungu vya sheria katika Mswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali za Sekta ya Sheria namba 3 wa mwaka 2023 na Mswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali namba 4 ya mwaka 2023 yenye lengo la kuboresha utekelezaji wa sheria mbalimbali nchini.

Ufafanuzi huo wa Serikali umetolewa na Mhe. Pauline Gekul Naibu Waziri wa Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi na Wataalam wa Wizara kwa kujibu hoja za Wabunge tarehe 23 Oktoba, 2023 kwenye kikao kati ya  Kamati na Wizara pamoja na Taasisi zake kilichofanyika ofisi za Bunge, Dodoma.

Katika kikao hicho, Kamati ilikuwa inasikiliza majibu ya Serikali kupitia majedwali ya ya Kamati, ambapo Kamati imepokea majibu ya Serikali na kuridhika kupitisha miswada hiyo yenye jumla ya sheria 33 zinazolenga kubadilishwa.

Awali akichangia katika kikao hicho Mjumbe wa Kamati Mhe. Abdullah Ali Mwinyi amesifu mabadiliko hayo kwani yamezingatia mambo mengi akitaja blue print kama mfano, jambo ambalo litafanya sheria zitakazobadilishwa kuishi muda mrefu kabla ya kuhitajika mabadiliko mengine.

Akitoa shukrani kwa Kamati Mhe. Gekul amefurahishwa na uamuzi wa Kamati kuridhia marekebisho hayo ambayo msingi wake ni kuboresha utendaji wa Serikali. “Ulimwengu unapobadilika mambo mengi yanajitokeza na hivyo kama nchi ni lazima kukabiliana na mabadiliko hayo, namna mojawapo ya kukabiliana na mabadiloko hayo ni mabadiliko ya sheria,” alisema.

Katika hatua nyingine Kamati hiyo imepokea taarifa ya utekelezaji kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Akichangia katika taarifa hizo Mhe. Mashimba Ndaki amesema umehimu wa Tume ya Hki za Binadamu na Utawala Bora unaongezeka kutokana na kuongezedka kwa idadi ya Watanzaniawa na kuongezeka kwa matukio ya uvunjanji wa haki za binadamu. Akashauri Tume kuwa na ofisi za Mikoa na Wilaya kuiwezesha kuwa karibu zaidi na wananchi katika kusimamia haki na utawala bora kwani makundi kama Sungu sungu na Walizi binafsi wakati mwingine hujichukulia hatua za kusimamia ulinzi huku wakikiuka haki za binadamu.

Akiahirisha kikao hicho Kaimu Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Florent Kyombo amesema Kamati yake kwa niaba ya Bunge itaendalea kushirikiana na Wizara na Taasisi zake katika kuimarisha utendaji wa Wizara ili kuisaidia Serikali kutimiza majukumu yake.