Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala, Katiba na Sheria Yahamasisha Wananchi wa Arusha Kujitokeza kwa Wingi Kampeni ya Mama Samia

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Joseph Kizito Mhagama, Mjumbe wa kamati hiyo Mhe. Joseph Thadayo amewasisitiza Wananchi wa Arusha kujitokeza kwa wingi na kutumia fursa iliyoletwa kwao na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria, ili kuweza kutatuliwa kero na changamoto zao za kisheria bila ya malipo.
Mhe. Thadayo ametoa rai hiyo alipopewa nafasi ya kutoa salamu za Kamati kwa niaba ya Bunge la Tanzania, wakati wa Uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwa Mkoa wa Arusha, Kampeni ambayo imezinduliwa Machi 28, 2025 kwenye viwanja vya Ngarenaro Jijini Arusha, ikitarajiwa kudumu kwa siku kumi mkoani humo.
Mhe. Thadayo vilevile amewataka Wanasheria na Mawakili wanaoshiriki kwenye Kampeni hiyo kutoka Serikalini na kwenye Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), kuzingatia maadili ya taaluma zao na kuhakikisha wanatenda haki kwa kila atakayekuwa anafika mbele yao kwa ajili ya kusikilizwa wakati wote wa utekelezaji wa Kampeni hiyo katika kutimiza dhamira njema ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa Watanzania.
Mbunge huyo pia amempongeza na kumshukuru Rais Samia kwa kuileta Kampeni hiyo, akimtaja kama kiongozi anayejiamini katika usimamizi wa Utawala wa Sheria, kwa kutaka Watanzania kujitambua na kufahamu Haki zao, suala ambalo amesema limekuwa likiwashinda Viongozi wengi Duniani.