Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria yaimwagia sifa Mahakama

Imewekwa: 14 Mar, 2023
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria yaimwagia sifa Mahakama

Na Lusajo Mwakabuku – WKS

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imekagua Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora na kuridhishwa kwa kazi inayofanywa na Mahakama katika utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya uboreshaji wa miundombinu ya majengo yake. 

Mara baada ya ziara hiyo ya siku moja ya ukaguzi wa utekelezaji wa Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora iliyofanyika tarehe 14 Machi, 2023, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe.  Florent Laurent Kyombo amesema kuwa Mahakama ni moja ya Taasisi inayofanya vizuri katika miradi yake ya ujenzi na hivyo kuwasihi Watumishi wa Mhimili huo kutoa huduma zinazoendana na uzuri wa miundombinu hiyo.

Akimwakilisha Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro katika Ziara hiyo, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul (Mb) aliishukuru kamati kwa pongezi hizo na kuahidi kutolea ufafanuzi kwa maandishi hoja na maswali yote yaliyoulizwa na Wajumbe wakati wa ziara hiyo na kuahidi kutekeleza ushauri kama ulivyotolewa na kamati.