Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Kamati Yaipongeza Wizara kwa Utekelezaji wa Mama Samia Legal Aid Campaign

Imewekwa: 21 Aug, 2023
Kamati Yaipongeza Wizara kwa Utekelezaji wa Mama Samia Legal Aid Campaign

Na George Mwakyembe, Emmanuel Msenga. Asia Mackenzie - WKS

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa jitihada inazozifanya katika kutekeleza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) ambayo imeendelea kuwa msaada mkubwa kwa wananchi hasa wale wa kipato cha chini katika kutatua changamoto zao za kisheria.

Akiongea kwenye kikao cha kupokea taarifa ya miezi mitatu ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara na Taasisi zilizo chini ya Wizara, tarehe 21 Agosti, 2023 Jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Joseph Mhagama (MB) amesema wameweza kubaini utekelezwaji mzuri kutokana na Wizara kuhakikisha inaishirikisha Kamati kila mkoa ambapo Kampeni hiyo inakuwa inazinduliwa.

“Sisi kama Kamati tunaipongeza sana Wizara kwa Kampeni yenu hii ya Mama Samia ya Msaada wa Kisheria na tunaridhishwa na utekelezaji wake mzuri na tumekuwa tukishirikishwa kila hatua na pia wananchi wamekuwa wakipongeza sana kwa kazi mnayofanya. Wananchi wetu wamekuwa wakitupigia simu na kushukuru kwa kuwasaidia kutatua changamoto zao, utekelezaji huu ni mzuri na sisi tutawaunga mkono kwa asilimia zote. Mwendelee kujipanga vizuri kwa mikoa mingine ili mfanye vizuri kama mlivyofanya kwenye mikoa ambayo tayari mmeisha tekeleza.” Alisema Mhe. Mhagama.

Naye Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul (MB) akimwakilisha Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro alisema katika mikoa minne ambayo tayari Wizara imeshapita wameshuhudia mengi ambayo yameipa Wizara uzoefu na mbinu mbadala katika kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na huduma za kisheria na elimu inapatikana kwa urahisi.

“Tayari Wizara imejipanga kwa mkoa wa Tabora ili kuhakikisha tunatekeleza Kampeni hii kwa ufanisi zaidi katika kutatua changamoto za kisheria zinazowakabili wananchi na Watanzania kwa ujumla. Lakini pia tumejipanga kutoa elimu ya sheria kwa wananchi ili kuwajengea uelewa mpana wa masuala ya kisheria,” aliongeza Mhe. Gekul.

Katika hatua nyingine, mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Boniface Nyangindu Butondo ambaye ni Mbunge wa Kishapu pia ameipongeza Wizara kwa utekelezaji mzuri wa Kampeni ya Mama Samia Msaada wa Kisheria. “Kampeni hii imekuwa muhimu sana kwa wananchi wetu, nimeona wakati wa utekelezaji wa Kampeni hii katika Jimbo langu la Kishapu. Kampeni hii iwe endelevu kwani inawasaidia sana wananchi na Kamati hii yote inawaunga mkono na wanafurahia jinsi utekelezaji unavyofanywa” Alisema Mhe. Butondo.

Vilevile, Mhe Butondo ameishauri Wizara ya Katiba na Sheria kupitia maeneo yote ambayo tayari Kampeni ya Mama Samia Msaada wa Kisheria imetekelezwa ili kupata mrejesho kama yale yote waliyoyaibua yamefanyiwa kazi na kutatuliwa kama vile utatuzi wa mirathi pamoja na migororo ya ardhi.

Akichangaia kwenye taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara na ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Mbunge wa Jimbo la Mlalo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Rashidi Shangazi ameipongeza Wizara kwa kubuni Kampeni hiyo ambayo imebeba jina la Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na maono yake. Pia Mhe. Shangazi ameitaka Wizara kuangalia namna gani wanajipanga ili kurekebisha miundombinu ya Mahakama ambayo imekuwa chakavu na kuwa siyo rafiki kwa wananchi.

Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ilizinduliwa Rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa tarehe 27 Aprili mwaka huu na hadi sasa imeshatekelezwa katika mikoa minne ambayo ni Dodoma, Manyara, Shinyanga na Ruvuma.