''KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA NI MKOMBOZI WA WANANCHI WA KONDOA''-NYANGASA
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma Mhe. Fatma Almas Nyangasa amesema maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuanzisha Kampeni ya Msaada wa Kisheria nchi nzima, imekuwa mkombozi kwa wananchi hasa wa pembezoni mwa nchi ambao hawana kipato cha kuweza kuzifuata huduma za Mahakama, kugharamia Mawakili pamoja na kuwapa maarifa wananchi ambao hawana uelewa juu ya masuala ya kisheria.
Mhe. Nyangasa amebainisha hayo leo Jumanne Mei 05, 2026 wakati akizungumza na Wananchi katika Uwanja wa Ubembeni Kata ya Kondoa Mjini, kuhusu ujio wa Kampeni hiyo ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika Wilaya ya Kondoa.
Amebainisha kuwa katika utendaji wa kila siku wa Ofisi yake changamoto kuu ni wananchi kutokuwa na uelewa wa kisheria, suala ambalo Kampeni hiyo itakwenda kuitatua kwa kiasi kikubwa.
"Ukienda kwa wananchi unagundua kuwa asilimia kubwa ya changamoto tulizonazo ni kwasababu wananchi kutojua wapi kwa kuanzia kwahiyo elimu hii inayotolewa katika Kampeni hii ni kitu cha muhimu na cha msingi sana kwa Watanzania na nikiri kuwa Mhe. Rais Samia aliona mbali katika hili kwasababu kama hujui taratibu ni ngumu sana kufikia kwenye utatuzi wa changamoto yako kwa haraka.
Niwahakikishie hii fursa ni muhimu sana kwetu wananchi wa Kondoa, naomba tuitumie vizuri" Amesema Mhe. Nyangasa.
Kwa upande Wakili wa Serikali kupitia Wizara ya katiba na Sheria na mratibu wa kampeni hiyo Wilaya ya Kondoa Everitt Magile Steph ameeleza kuwa changamoto kubwa waliyoikuta kwa wananchi wa Wilaya hiyo inasababishwa na migogoro ya ardhi.
Ametoa rai pia kwa wananchi wa Wilaya hiyo wenye changamoto mbalimbali za kisheria kufika kwenye vituo vya kutolea huduma ili kuweza kuhudumiwa mpaka kufikia tarehe Mei 15, 2026, zoezi hili litakapokamilika.