KATIBA NA SHERIA, UN WOMEN KUIMARISHA USHIRIKIANO
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women) Tanzania, Bi. Julia Broussard, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika kuhakikisha wanawake nchini wanapata haki na huduma za msaada wa kisheria kwa wakati.
Katika mazungumzo hayo, yaliyofanyika jijini Dodoma, pande hizo zimejadili maeneo mbalimbali ya ushirikiano yanayolenga kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wanawake, hususan kupitia mifumo ya msaada wa kisheria na matumizi ya teknolojia katika kurahisisha upatikanaji wa taarifa na huduma za kisheria.
Miongoni mwa maeneo yaliyobainishwa ni kuimarisha mifumo ya utoaji wa msaada wa kisheria, ikiwemo kutumia teknolojia za kisasa kuwafikia wananchi kwa ufanisi zaidi na kuongeza upatikanaji wa taarifa kuhusu haki za wanawake.
Aidha, mazungumzo hayo yameangazia umuhimu wa kujenga uwezo kwa watoa huduma za msaada wa kisheria na wadau mbalimbali, wakiwemo Mawakili wa Serikali, ili kuwawezesha kushughulikia kwa ufanisi masuala yanayohusu haki na mahitaji ya wanawake.
Kwa upande wake, UN Women imeeleza utayari wa kuendelea kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria katika maeneo yenye maslahi ya pamoja, ikiwemo kuimarisha mifumo inayowezesha wanawake kupata haki, taarifa sahihi za kisheria na huduma stahiki.
Katika mazungumzo hayo, Mkurugenzi Mkazi wa UN Women Tanzania, Bi. Julia Broussard, aliambatana na Naibu Mkurugenzi Mkazi, Bi. Karen Giathi.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza ufanisi katika juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi, hususan wanawake, wanapata huduma za kisheria na haki bila vikwazo, sambamba na kuimarisha mifumo ya utoaji haki nchini.