Katiba na Sheria Yawakutanisha Wadau Kujadili Utekelezaji wa Mikataba ya Haki Za Binadamu

Wizara ya Katiba na Sheria kupitia Idara ya Haki za Binadamu imewakutanisha wadau mbalimbali kutoka Bara na Zanzibar katika kikao kazi cha kukamilisha taarifa ya Nchi ya kufuatilia utekelezaji wa Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu pamoja na Mkataba wa Haki za Wanawake Barani Afrika (Itifaki ya Maputo).
Katika kikao hicho kinachofanyika kuanzia tarehe 22 hadi 25 Oktoba, 2024 Flomi hoteli mjini Morogoro, kitaandaa taarifa itakayoonesha ni kwa namna gani kwa mujibu wa Mikataba tajwa Nchi ya Tanzania imefanikiwa kutekeleza viwango ambavyo Nchi inapaswa kuvifuata katika kuendeleza na Kulinda Haki za Wanawake.
Itifaki ya Maputo imekuwa na manufaa makubwa katika kuwezesha na kuendeleza upatikanaji wa Haki pamoja na kuonesha jitihada zinazofanywa na Serikali katika kutokomeza vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya Wanawake nchini Tanzania.
Tanzania ni miongoni mwa Nchi ambazo zimeridhia utekelezaji wa Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu pamoja na Mkataba wa Haki za Wanawake barani Afrika (Itifaki ya Maputo) yenye malengo ya kulinda Haki za Wanawake inayojumuisha Haki za kushiriki katika siasa, kazi za kijamii ,Haki ya uzazi na kupinga mila potofu kama vile ukeketaji.