Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

MAENEO YENYE CHANGAMOTO ZA KISHERIA YAAINISHWE MAPEMA KUWAFIKIA WANANCHI

Imewekwa: 27 Oct, 2026
MAENEO YENYE CHANGAMOTO ZA KISHERIA YAAINISHWE MAPEMA KUWAFIKIA WANANCHI

Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Bw. Richard Kayombo, amewahimiza wataalamu watakaotekeleza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) Awamu ya Pili kuainisha mapema maeneo yenye changamoto kubwa za kisheria pamoja na makundi ya wananchi yaliyo katika hatari ya kukosa huduma hizo ili yaweze kupewa kipaumbele katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria.

Bw. Kayombo ametoa wito huo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wataalamu watakaoshiriki katika utekelezaji wa kampeni hiyo mkoani Pwani, inayotarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 28 Oktoba, 2026, akisisitiza kuwa maandalizi mazuri ni msingi muhimu wa kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi wanaozihitaji zaidi.

Amesema ni muhimu kwa wataalamu kufanya tathmini ya changamoto za kisheria zinazowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali ili kuwezesha huduma kutolewa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya jamii. Hatua hiyo itasaidia kuhakikisha wananchi wenye changamoto za kisheria wanapata fursa ya kupata ushauri na msaada wa kisheria kwa wakati.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wataalamu kutumia ujuzi na maarifa watakayopata kupitia mafunzo hayo katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, weledi na kuzingatia misingi ya haki, usawa na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Awamu ya Pili inalenga kusogeza huduma za msaada wa kisheria karibu na wananchi, kuongeza uelewa kuhusu haki na wajibu wao kisheria na kuwawezesha kupata suluhisho la changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili.