Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

ULEGA ASISITIZA UMUHIMU WA UTAWALA BORA KAMA NGUZO MUHIMU YA KUDUMISHA AMANI, UTULIVU NA MAENDELEO ENDELEVU

Imewekwa: 27 Oct, 2026
ULEGA ASISITIZA UMUHIMU WA UTAWALA BORA KAMA NGUZO MUHIMU YA KUDUMISHA AMANI, UTULIVU NA MAENDELEO ENDELEVU

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega, amesisitiza kuwa Utawala Bora unahusisha kusikiliza wananchi, kushughulikia malalamiko yao kwa wakati, kuwajibika na kuwashirikisha katika masuala yanayowahusu, akieleza kuwa misingi hiyo ni nguzo muhimu katika kudumisha amani, utulivu na kuharakisha maendeleo endelevu nchini.

Waziri Ulega ameyasema hayo leo, Oktoba 26, 2026, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Uraia na Utawala Bora kwa Viongozi na Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa mkoani Manyara. 

Waziri Ulega amesisitiza kwamba  Utawala Bora ni pamoja na  kuhakikisha wananchi  wanasikilizwa  malalamiko yao kwa wakati, pamoja na kutoa mrejesho kuhusu hatua zilizochukuliwa ili kuimarisha uwajibikaji na kujenga imani ya Wananchi kwa Serikali yao.

Amesema kuwa kuimarisha misingi ya Utawala Bora kunahitaji Viongozi na Watendaji kuweka kumbukumbu sahihi za malalamiko yanayopokelewa, hatua zinazochukuliwa na mrejesho unatolewa  kwa wananchi, ili kuhakikisha kero zao zinafuatiliwa na kutatuliwa kwa ufanisi. Ameeleza kuwa, utaratibu huo utapunguza urudiaji wa malalamiko na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa umma.

Aidha, Waziri Ulega amesema mafunzo hayo yanaakisi falsafa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kufanya kazi kwa kuzingatia utu, akiwataka viongozi na watendaji kutambua madaraka waliyopewa ni dhamana inayopaswa kutumiwa kwa manufaa ya umma na kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi.

“Ushiriki wa wananchi unahitaji taarifa. Wananchi wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika mambo yanayowahusu, ikiwemo mipango ya maendeleo, ili waweze kuelewa, kuchangia na kuwa sehemu ya maamuzi yanayogusa maisha yao,” amesema Waziri Ulega.

Amesisitiza kuwa mawasiliano yenye ufanisi kati ya Serikali na wananchi ni muhimu katika kuimarisha Utawala  Bora  na kuzuia migogoro isiyo ya lazima. Ameongeza kuwa wananchi wanaposikilizwa, kushirikishwa katika maamuzi na kupata ufumbuzi wa kero zao kwa wakati, huimarisha mahusiano kati yao na viongozi wao, hali inayochangia kudumisha amani na utulivu katika jamii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Martine Shigela  ameshukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuendelea kutoa mafunzo ya Uraia na Utawala Bora kwa Viongozi na Watendaji wa Serikali, akieleza kuwa mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka ambao Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan,  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  ikisisitiza masuala ya Utawala Bora, uzingatiaji wa Sheria na umuhimu wa kuzingatia utu katika utendaji kazi 

Awali akitoa takwimu  za utekelezaji wa mafunzo hayo kwa kipindi cha miaka miwili 2024/2025 na mwaka  wa fedha 2025/2026, Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Seif Shekalaghe amesema, katika miaka miwili  jumla ya Viongozi na Watendaji 8,340 walipatiwa mafunzo katika Halmashauri 133  zilizopo katika Mikoa  20. 

Wizara inaendelea kutekeleza Mpango wa utoaji elimu hiyo ambapo kwa mwaka 2026/2027 Mkoa wa Manyara  umekuwa ni Mkoa wa kwanza kupatiwa mafunzo hayo na inatarajia kuwafikia Watendaji 1,003 katika Mkoa huo.