"KUIMARIKA KWA SEKTA YA SHERIA UKANDA WA AFRIKA MASHARIKI-CHACHU YA UPATIKANAJI HAKI"
Ushirikiano wa kikanda kupitia vyama vya kitaaluma katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Sheria vinaonesha dhamira ya dhati ya wanachama wake kubadilisha uzoefu,kujenga uwezo na kuwa na viwango bora vya utoaji huduma kwa wanachama wake katika kuwahudumia wananchi.
Kwa mantiki hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Eliakim Maswi leo tarehe 20, Februari 2026, Mtumba jijini Dodoma, amekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Chama cha Mawakili wa Afrika Mashariki ukiongozwa na Katibu wa Chama hicho Wakili John Seka.
Mazungumzo hayo yameonesha dhamira ya dhati ya kuimarisha sekta ya Sheria katika ukanda wa Afrika Mashariki mkazo ukiwa katika utoaji wa elimu ya kisheria kwa umma na msaada wa kisheria kwa wananchi wasiojiweza.
Katika mazungumzo hayo, Pande zote mbili zimejadili namna bora ya kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali katika utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala (ADR) na katika kufanya majadiliano ya mikataba ili kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma na kulinda maslahi ya Taifa.
Katika hatua nyingine Uongozi wa Chama hicho umeishukuru Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kwa kufanikisha upatikanaji wa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ya Chama hicho ambacho kwa sasa kina jumla ya Mawakili elfu 45,000 .
Hatua hiyo inaonesha kukua kwa taaluma ya Sheria na fursa za ushirikiano wa kikanda jambo ambalo linatarajia kuleta manufaa makubwa kwa jamii, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za kisheria,kupunguza migogoro kupitia utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala.
Ikumbukwe kuwa Wizara ya Katiba na Sheria hivi karibuni imeingia makubaliano na taasisi mbalimbali katika utoaji wa huduma za kisheria ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wote na huduma za kisheria zinaboreshwa kwa ustawi wa wananchi.