MAWAKILI, MAAFISA ARDHI WANOLEWA KUSIMAMIA MIKATABA YA RASILIMALI
Wizara ya Katiba na Sheria imetoa mafunzo ya Usimamizi wa mikataba ya uwekezaji hususani katika mali na rasilimali asilia za nchi kwa baadhi ya Mawakili wa Serikali na Maafisa Ardhi wa Halmashauri za Wilaya za mkoa wa Dodoma kwa lengo la kuwaongezea uelewa kuhusu mifumo ya kisheria na kitaasisi inayosimamia mikataba hiyo, pamoja na kuhakikisha mikataba hiyo inaandaliwa, inatekelezwa na kusimamiwa kwa kuzingatia sheria, taratibu na maslahi ya Serikali.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Uangalizi wa Utajiri Asili na Maliasilia, Bw. Everest Mashiba, amesema mafunzo haya kwa Mawakili wa Serikali na Maafisa Ardhi ni muhimu katika kuhakikisha mikataba inayohusu mali na rasilimali za nchi inasimamiwa kwa weledi na kwa kuzingatia matakwa ya sheria.
“Mafunzo haya yatasaidia kujenga uelewa wa pamoja na kuimarisha mifumo ya kitaasisi katika ngazi za Halmashauri, hususan katika eneo la usimamizi wa masuala ya ardhi, uwekezaji, mali na rasilimali asilia” alisema Mashiba.
Mashiba mesema wakati wa mafunzo haya washiriki watapata fursa ya kujadiliana masula mbalimbali yanayohusu mikataba ya kukuza na kulinda uwekezaji, ikiwemo masharti ya mikataba, ulinzi wa mali na rasilimali za nchi, pamoja na namna bora ya kufuatilia utekelezaji wa mikataba hiyo pamoja na kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji na usimamizi wa mikataba ya uwekezaji.
Mafunzo hayo yanatolewa ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali katika kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na usimamizi madhubuti wa mikataba ya uwekezaji, huku ikilenga kuhakikisha maslahi ya nchi yanalindwa sambamba na kuweka mazingira wezeshi kwa uwekezaji wenye tija.