BODI YA MSAADA WA KISHERIA YATAKIWA KUFANYA UPIMAJI NA UFUATILIAJI WA CHANGAMOTO ZA KISHERIA ZINAZOIBULIWA MSLAC.
Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mh. Dkt Juma Homera, ameiagiza Bodi ya Kitaifa ya Ushauri ya Msaada wa Kisheria kuweka utaratibu wa kupima na kutoa mrejesho kwa jamii kupitia vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa huduma na utatuzi wa changamoto zinazotatuliwa kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.
Waziri Dkt. Homera ametoa agizo hilo tarehe 21 Septemba, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo elekezi kwa bodi mpya ya kitaifa ya ushauri wa msaada wa kisheria.
“Kila msaada mnaoutoa ufikie malengo, muwe na utaratibu wa kupima yale ambayo mmeyapokea yametekelezwa mangapi na yamebakia mangapi ili jamii ione na muyatangaze ili jamii ijue”. Alisema Dkt. Homera.
Aidha Waziri Dkt. Homera ameisisitiza bodi kuhakikisha wanaendeleza mipango iliyowekwa na bodi iliyomaliza muda wake ukiwemo mpango wa kuanzisha Sheria tv na redio ambao utasaidia elimu ya kisheria kuwafikia wananchi wengi zaidi na kusaidia kupunguza gharama.
Awali akimkaribisha Mhe. Waziri Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Seif Shekalaghe, alisema mafunzo hayo elekezi yanalenga kuhakikisha wajumbe wa bodi wanafahamu majukumu na mipaka yao ya utendandaji kazi pamoja na muundo wa utendaji kazi wa Wizara.
Akitoa shukrani kwa Mh. Waziri, mwenyekiti wa bodi hiyo Jaji Mstaafu Crecencia Makuru amemuhakikishia Mh. Waziri kuwa wako tayari kufanya kazi na watatumia umahiri na uzoefu wao kuhakikisha wanashauri namna bora ya kuboresha huduma, na watazingatia sheria, kanuni na miongozo kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na huduma.
Bodi hiyo mpya ya kitaifa ya ushauri wa msaada wa kisheria imeteuliwa tarehe 29 Juni, 2026 na itafikia ukomo wa ufanyaji kazi tarehe 28 Juni, 2029 na inaundwa kwa mujibu wa Sheria ya Msaada wa Kisheria, Sura ya 21.