Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Maafisa wa Ustawi wa Jamii ni Wadau Muhimu wa Wizara ya Katiba na Sheria – Gekul

Imewekwa: 06 Sep, 2023
Maafisa wa Ustawi wa Jamii ni Wadau Muhimu wa Wizara ya Katiba na Sheria – Gekul

Na Lusajo Mwakabuku & Candid Nasua – WKS Dodoma

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul amesema Wizara kupitia Taasisi zake zikiwemo Mahakama ya Tanzania, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu kwa pamoja zimekuwa zikifanya kazi kwa ukaribu na Maafisa wa Ustawi wa Jamii katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mhe. Naibu Waziri ameyasema hayo wakati akimwakilisha Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Maafisa Ustawi wa Jamii ulioandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, tarehe 06 Septemba, 2023 Jijini Dodoma.

Akitoa salaam za Wizara katika mkutano huo, Mhe. Gekul alielezea namna ambavyo Wizara imekuwa ikishirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii hususan katika utekelezaji wa Sheria mbalimbali ikiwemo Sheria za Ndoa mwaka 1971, Sheria ya Mtoto mwaka 2009 na Kanuni ya Adhabu iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Pamoja na hayo, aliongeza kuwa, Wizara kupitia wataalam iliwasilisha maoni yao wakati wa mchakato wa upatikanaji wa Mwongozo wa Taifa wa uendeshaji, usimamizi na uratibu wa Mabaraza ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa mwaka 2023 ambao leo hii ni moja ya Miongozo iliyokuwa inazinduliwa wakati wa Mkutano huu.

Mhe. Gekul aliongeza kuwa Wizara ya Katiba na Sheria ni mdau mkubwa wa masuala ya Ustawi wa Jamii, na kwamba Wizara inaunga mkono jitihada zote zinazochukuliwa na Serikali kuhusu masuala ya ustawi wa jamii ikiwepo kusimamia Sheria mbalimbali ikiwemo mchakato wa kukamilisha maboresho ya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, ambao upo mbioni kukamilika na kwamba Wizara ina imani kabisa mchakato wa mabadiliko utakamilika hali itakayomsaidia kumwepusha mtoto wa kike na madhila yakuolewa katika umri mdogo.

Katika mkutano huo Mhe. Naibu Waziri alimwakilisha Mhe. Waziri wa Katiba na Sheria naye Mhe. Dkt. Dotto Biteko Naibu Waziri Mkuu alimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philipo Isdor Mpango.