Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Maamuzi ya Mahakama hayaangalii unyonge wa mtu

Imewekwa: 25 Jul, 2023
Maamuzi ya Mahakama hayaangalii unyonge wa mtu

Na William Mabusi – WKS Tunduru

Timu inayotekeleza Mama Samia Legal Aid Campaign Wilayani Tunduru katika Mkoa wa Ruvuma imesema maamuzi ya Mahakama hayatolewi kwa kuangalia fulani ana uwezo na kumpa haki hata kama yeye ndiye mwenye makosa bali haki hutolewa kwa mujibu wa sheria na kadri ushahidi ulivyotolewa.

Hayo yamesemwa na Wakili Jane Lyimo kutoka Wizara ya Katiba na Sheria wakati akitoa mada ya sheria kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya ofisi za Kata ya Nanjoka Wilayani Tunduru tarehe 24 Julai, 2023.

 “Maamuzi ya Mahakama hayaangalii mtu mwenye uwezo apewe haki na yule asiye kuwa na uwezo kunyang'anywa haki yake. Hali ya unyonge wa mtu haisababishi yeye kukosa haki yake kisheria.” Alisema Bi. Lyimo.

Aidha, Bi. Lyimo aliwashauri wananchi kama wana uthibitisho wa matukio yenye viashiria vya rushwa kutoa taarifa hizo kwenye vyombo vingine vya haki kama TAKUKURU na Polisi.

Akichangia mada hiyo Mhe. Jane Pascal Mudogo Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Nakapanya amesema sheria inaruhusa mtuhumiwa kubadilishiwa Hakimu endapo hana imani naye lakini pia Mahakama imeanzisha Madawati ya kupokea malalamiko ili wananchi wanaokutana matukio yenye viashiria vya rushwa kutoa taarifa hizo huko.

Mkutano huo uliwahusisha wananchi kutoka Vijiji vya Nanjoka, Uwanja wa ndege na NHC, ulifanyika ofisi za Kata ya Nanjoka, Halmashauri ya Tunduru ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Mama Samia inayolenga kutoa elimu ya sheria na msaada wa sheria kote nchini.

Baadaye timu hiyo ilitembelea shule ya Sekondari ya Frank na shule ya Msingi Nanjoka kutoa elimu juu ya haki na wajibu wa mtoto pamoja na mada kuhusu ukatili wa kijinsia. Akitoa shukrani kwa timu ya Mama Samia Legal Aid Campaign kutoa elimu hiyo shuleni kwao mwanafunzi Salma Mbunya wa darasa la tano alisema “nawashukuruni kwa kutupa elimu ya mambo ya ukatili wa kijinsia ambayo tukikutana nayo tunajua wapi pa kupata msaada nasisi tutatoa elimu hiyo kuwaelimisha wenzetu.”