Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Mabaraza ya Usuluhishi ya Kata yapewe mafunzo ya mara kwa mara

Imewekwa: 26 Jul, 2023
Mabaraza ya Usuluhishi ya Kata yapewe mafunzo ya mara kwa mara

Na William Mabusi – WKS Tunduru

Wanakijiji cha Masugulu Kata ya Marumba wameomba Serikali kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara Wajumbe wa Mabaraza ya Usuluhishi ya Kata kuwawezesha kufanya jukumu la usuluhishi kwa ufanisi na hivyo kusaidia kumaliza migogoro mbalimbali ikiwemo ya ardhi kwenye ngazi za Kata.

Ushauri huo umetolewa kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika tarehe 25 Julai, 2023 kwenye vijiji vya Masugulu na Marumba ambapo elimu ya Ndoa na talaka, Mirathi na wosia, Ukatili wa kijinsia na Ardhi ilitolewa na Timu ya Mama Samia Legal Aid Campaign ikifuatiwa na huduma ya msaada wa sheria kwa mwananchi mmoja mmoja.

Akichangia kwenye mada ya ardhi mzee Issa Zuberi Ngonyani kutoka Kijiji cha Masugulu amesema, “kwenye Baraza la Usuluhishi la Kata kuna shida kwani wanaochaguliwa hawana elimu ya sheria na hivyo miongoni mwao wanasumbua na kushindwa kutimiza jukumu lao la usuluhishi na wanafanya hayo kwa kuwa sheria hawazijui zaidi ya kujua mila na desturi za eneo husika.”