Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Mafunzo ya ulinzi wa watoa taarifa na mashahidi yafanyika Dodoma.

Imewekwa: 30 Jun, 2023
Mafunzo ya ulinzi wa watoa taarifa na mashahidi yafanyika Dodoma.

Na George Mwakyembe – WKS

Wizara ya Katiba na Sheria imefanya mafunzo juu ya Sheria na Kanuni za watoa taarifa na mashahidi kwa Maafisa mbalimbali kutoka taasisi za haki jinai tarehe 30 Juni, 2023 Jijini Dodoma yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kumlinda mtoa taarifa   na ushahidi  wakati wa kutekeleza majukumu ya Serikali.

Akiwasilisha mada, Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Khalist Luanda amesema “Sheria ya kumlinda mtoa taarifa na ushahidi lazima izingatiwe kwani ni Sheria ambayo itasaidia kupunguza masula ya uhalifu kwa sababu taarifa zao zitakuwa zinatolewa na kufanyiwa kazi lakini kanuni hizi zinamlinda mtoa taarifa. Mnaagizwa kuzitekeleza na kuzifuata ipasavyo kwa sababu ninyi ndiyo wapokeaji taarifa za haki jinai.”

Aidha, Bw. Luanda amesema changamoto kubwa inayojitokeza kwenye Sheria hiyo ni wapokeaji taarifa kutotunza siri baada ya kupokea taarifa kitu ambacho kimekuwa changamoto sana kwani inaleta udhaifu wa namna ya kukabiliana na wahalifu baada ya kupokea taarifa. Kwa Kanuni na Sheria hii inaruhusu utanzaji wa siri ili mtoaji wa taarifa alindwe.

Mada hiyo ya kanuni inayoitwa The Whistleblower and Witness Protection Regulations, 2023 inaelezea namna ya kulinda usalama wa mtu anayetoa taarifa za uhalifu na kanuni hiyo inasomwa pamoja na sheria ya The Whistleblower and Witness Protection Act (Cap.446).

Akichangia kwenye mafunzo hayo ndugu John Kidando kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema sheria hiyo ni muhimu sana kwa sababu inamlinda na kumpa haki mtu anayetoa taarifa, iwapo mtu aliyetoa taarifa atatakiwa kupewa zawadi baada ya kutoa taarifa basi atatakiwa kupewa kwa kulindwa pasipo kutoa taarifa zake.

Mafunzo hayo yamehudhuriwa na maafisa kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Rais TAMISEMI, pamoja na Maafisa wa Polisi kutoka mkoa wa Dodoma ambao wote ni walengwa wakubwa katika kupokea taarifa mbalimbali za uhalifu na zenye manufaa kwa Taifa.