Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

MAGEUZI YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA NA TAASISI ZAKE YAIKOSHA KAMATI YA BUNGE

Imewekwa: 28 Mar, 2026
MAGEUZI YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA NA TAASISI ZAKE YAIKOSHA KAMATI YA BUNGE

Kamati  ya Kudumu  ya  Bunge  ya Utawala, Katiba na Sheria ikiongozwa na  Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo  Mhe. Edwin Enosy  Swalle  imeridhia na kuipitisha Randama ya Mpango na Bajeti  kwa mwaka  wa fedha 2026/2027 ya Wizara ya Katiba na Sheria na taasisi zake katika kikao kilichofanyika leo tarehe 28 Machi, 2026 Bungeni jijini, Dodoma.

Randama hiyo imesheheni vipaumbele   vilivyojikita katika kuimarisha sekta ya Sheria  kwa kufanya mageuzi ya kiutendaji na uwajibikaji kwa  kuifanya kuwa  mhimili mkuu wa maendeleo ya Taifa kufikia Dira 2050.

Wajumbe wa Kamati katika nyakati tofauti tofauti wameipongeza Wizara na Taasisi zake  kwa jitihada za kiubunifu zinazofanyika katika kuimarisha huduma za upatikanaji wa haki kwa Watanzania kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia , na programu ya "Sema na Waziri" ambapo wananchi wanaweza kupata huduma za kisheria kwa kupiga simu katika kituo cha huduma kwa mteja cha wizara bila malipo.

Kuwasilishwa na kuidhinishwa kwa  Randama hiyo ni  hatua  muhimu kuanza kwa  maandalizi ya  mwisho  ya  Hotuba ya Bajeti  itakayowasilishwa  rasmi  katika Mkutano  wa Bunge la Bajeti la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linalotarajiwa kuanza  karibuni.