Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Mahakama Kuendelea na Utekelezaji wa Mpango wa Ujenzi wa Mahakama Nchini – Mhe Gekul

Imewekwa: 31 Aug, 2023
Mahakama Kuendelea na Utekelezaji wa Mpango wa Ujenzi wa Mahakama Nchini – Mhe Gekul

Na. George Mwakyembe - WKS DODOMA.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul ameeleza kuwa Mahakama inaendelea na mpango wa kujenga ofisi za Mahakama nchini kote na kwamba hadi sasa ofisi 18 za Mahakama za Wilaya zimeshajengwa na Mahakama za Mwanzo 71. Mahakama hizi zinajengwa kwa utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24

Mhe. Gekul ameyasema hayo leo tarehe 30 Agosti, 2023 bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tunduru Kusini Mhe. Daimu Idd Mpakate ambaye aliuliza lini Mahakama itajenga Mahakama za Mwanzo katika Tarafa ya Nalasi, Lukumbule, pamoja na Tarafa ya Namasakata.

Pia, Mhe. Gekul amefafanua kuwa tayari Mahakama ya Mwanzo ya Nalasi inajengwa katika mwaka wa fedha 2023/24 ikiwa ni sehemu ya ujenzi wa Mahakama 71 za mwazo ambazo zitajengwa nchi nzima na tayari Mshauri elekezi ameanza kazi na ujenzi utaanza Oktoba 2023. Vilevile, Mhe. Gekul ameleza kuwa katika mwaka wa fedha 2023/24 moja ya Mahakama za Wilaya zitakazojengwa ni Mahakama ya Wilaya ya Tunduru.

Aidha, Mhe. Gekul ameeleza kuwa Mahakama nchini ina magari mawaili ya (Mobile Court) ambayo yamekuwa yakihudumia Mikoa yenye watu wengi ambayo ni Kagera, Tanga, Arusha, Morogoro, Dar es Salaam.  Mbali ya hizo Mobile Courts kuwa msaada mkubwa katika kupunguza malimbikizo ya kesi, gharama za kuziendesha ni kubwa hivyo mpango wa Serikali ni kujenga Mahakama ili kupunguza gharama za uendeshaji.

Pia Mhe. Gekul alifafanua zaidi jinsi Serikali ilivyojipanga kujenga Mahakama za Wilaya  18 na  ambazo  zitajengwa kwa mwaka wa fedha 2023/24 na miongoni mwa Mahakama hizo ni Mahakama ya Wilaya ya Mbulu ambayo miundombinu yake imechakaa pamoja na Mahakama za Wiliya zingine. Mahakama hizi zinajengwa ikiwa ni utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24.