Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Mahakama ya Mwanzo ya Tarafa ya Bwakila Kujengwa – Mhe. Gekul

Imewekwa: 08 Nov, 2023
Mahakama ya Mwanzo ya Tarafa ya Bwakila Kujengwa – Mhe. Gekul

Na George Mwakyembe - WKS Dodoma.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul amefafanua kuwa Serikali katika mwaka fedha 2023/24 imejipanga kujenga Mahakama zaidi ya 60 nchini ikiwemo Mahakama ya Mwanzo ya Tarafa ya Bwakila.

Mhe. Gekul ameyasema hayo tarehe 07/11/2023 bungeni Jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Morogoro Kusini Mhe. Innocent Edward Kalongoles aliyetaka kujua ujenzi wa Mahakama katika eneo hilo utafanyika lini. Mhe. Gekul amefafanua kuwa tayari zabuni imetangazwa kwa ajili ya kumpata Mkandarasi wa ujenzi wa Mahakama hiyo na wakati wowote atatangazwa na kuanza kazi.

Aidha, Mhe. Gekul ameeleza kuwa Mahakama ya Mwanzo ya Matombo na Namvua zina majengo ambayo ni chakavu na tayari Serikali imeyaweka katika mpango wa ukarabati katika mwaka wa fedha 2024/25 mpango ambao utajumisha ukarabati wa Mahakama zingine nchini.

Pia Mhe. Gekul ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa zaidi ya shilingi bilioni 88 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa Mahakama ili haki ipatikane kwa wakati. Hivyo amemtoa wasiwasi Mbunge huyo wa Mororgoro Kusini na kuahidi kuwa Mahakama hiyo itajengwa kwa wakati.