MAJAJI NA MAHAKIMU WANAWAKE WAASWA KUWA MFANO BORA KWA MAENDELEO YA SEKTA YA SHERIA NCHINI

Majaji na Mahakimu Wanawake nchini wameaswa kuwa mfano wa majaji na mahakimu bora nchini kwa kufanya kazi kwa bidii pamoja na kujengeana uwezo baina yao ili waongeze kasi ya maendeleo katika sekta ya Sheria nchini.
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Eliakim Maswi ametoa rai hiyo Septemba 15, 2025 katika ukumbi wa Mikutano wa ofisi hiyo Mtumba Dodoma, alipotembelewa na Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) na kufanya kikao cha pamoja na menejimenti ya wizara.
"Wanawake wakiwaona ninyi mko katika ngazi za juu za sekta inayoshughulikia utoaji wa haki wanapata Imani kubwa kuwa wana wawakilishi wao, nawasihi muwe majaji na mahakimu bora nchini, mjengeane uwezo baina yenu na pia uwepo wenu sio tu ishara ya usawa bali uwe nguzo ya ustawi wa maendeleo ya taifa'', amesema Maswi.
Mwenyekiti wa TAWJA Mhe Jaji Barke Sehel ameishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa ushirikiano baina yao huku akianisha maeneo ya ushirikiano zaidi hususani katika utoaji wa elimu kwa umma kuhusu masuala ya rushwa ya ngono kwakuwa baadhi ya mipango yao ni kukuza haki za binadamu na usawa kwa wote.
"Tunaomba Wizara iangalie namna ya kuongeza ushirikiano na TAWJA kwani tuna mpango mkakati wa kukuza haki za binadamu na usawa kwa wote hasa wanawake, wasichana na makundi maalumu Pamoja na kubuni na kuunga mkono shughuli za kupinga na kuondoa aina zote za ukatili na dhuluma", amesema Mhe. Jaji Sehel.
Aidha maeneo ya ushirikiano baina ya TAWJA na Wizara ya Katiba na Sheria yaliyo ainishwa ni pamoja na kushirikiana katika maeneo ya haki za binadamu, Msaada wa Kisheria, Usimamizi wa Sheria za Utajiri Asili na Maliasilia za nchi na utoaji wa elimu ya Katiba na uraia.