Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Makondo Ataka Umakini Dawati la Huduma za Kisheria

Imewekwa: 16 May, 2024
Makondo Ataka Umakini Dawati la Huduma za Kisheria

Na Lusajo Mwakabuku – WKS Dodoma.

Wizara ya Katiba na Sheria imeanzisha Dawati Maalum la huduma za kisheria katika ofisi za Wizara hiyo kwa lengo la kutatua kero za wateja wenye malalamiko juu ya huduma za kisheria zinazotolewa katika mifumo mbalimbali ya utoaji haki.

Akizungumza na baadhi ya watumishi wa Wizara wanaotoa huduma katika dawati hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Gasper Makondo alisema dawati hilo litarahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi hasa wale wanaofika Wizarani kwa ajili ya msaada zaidi.

Aidha Bi. Makondo aliongeza kuwa wananchi wana imani kubwa na Serikali hasa kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia hivyo kila mtumishi ana wajibu wa kuhakikisha kuwa anafanya kazi kwa uadilifu kwa lengo la kuwasaidia wananchi hasa wale wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za Mawakili na hatimaye watimize maono ya Rais Samia juu ya wananchi wote kupata haki.

“Wapo watu wana matatizo na wanahangaika kupata msaada wa kisheria lakini hawajui waanzie wapi, wafanye nini ili kupata huduma hii. Tumeanzisha dawati hili ili mteja atakayefika wizarani aweze kupata huduma bila ya kupoteza muda mrefu kuzunguka maofisini hasa kwa changamoto ambazo nyingi zinahitaji uelewa zaidi. Hivyo hakikisheni mnatoa huduma kiuweledi ili tuweze kuwasaidia wananchi.” Alisema Bi. Makondo.

Aidha, Katibu Mkuu huyo alitoa rai kwa watumishi wanaowapokea wateja wanaofika wizarani hapo kwa ajili ya huduma kuhakikisha kuwa wanatumia lugha nzuri, busara na kutoa huduma ndani ya muda mfupi kwani wananchi wanaofika wizarani tamanio lao ni kuona matatizo yao yatapatiwa ufumbuzi.

“Ninapokea wananchi wengi kila siku na wapo wanaotokea maeneo ya mbali kabisa wanasafiri kwa tabu ila wakiamini kuwa  wakifika hapa wizarani wameleta changamoto zao sehemu sahihi. Sasa tunapowahudumia tukumbuke gharama na muda walioutumia mpaka kufika hapa badala ya kuwapa majibu mepesi ambayo hayawasaidii katika changamoto zao.” Aliongeza Bi. Mary Makondo.

Dawati hili ni muendeleo wa mbinu mbalimbali ambazo Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kuzibuni katika kuhakikisha huduma za kisheria zinawafikia wananchi katika njia rahisi zaidi na zinazopunguza gharama na usumbufu kwa mwananchi.