Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Makondo: Tushirikiane Kutunza Amani

Imewekwa: 12 Oct, 2023
Makondo: Tushirikiane Kutunza Amani

Na William Mabusi – WKS Morogoro

Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo ameitaka jamii kuwa mstari wa mbele katika kufichua uhalifu kwa lengo la kuendeleza amani na usalama kwa maslahi mapana ya taifa.

Bi. Makondo ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya Sheria ya Ulinzi wa Watoa Taarifa na Mashahidi ya mwaka, 2015 (The Whistleblower and Witness Protection Act, 2015) na Kanuni zake za mwaka 2023 kwa Maafisa Uchunguzi Waandamizi kutoka Taasisi zinazotekeleza sheria hiyo, tarehe 12 Oktoba, 2023 Mkoani Mororgoro.

“Uwepo wa matukio ya uhalifu kunaondoa amani kwenye jamii na husababisha maendeleo kwa namna fulani kusimama hivyo tushirikiane kwa pamoja kutokomeza uhalifu ili shughuli za maendeleo ziendelee kufanyika katika sekta zote; kilimo, ufugaji, huduma na biashara,” Alisema.

Msisitizo mkubwa wa mafunzo hayo ni kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya usalama wao baada ya kutoa taarifa na ushahidi wa kutokea au uwezekano wa kutokea kwa uhalifu.

“Wananchi wakiwa na uhakika wa usalama wao katika kutoa taarifa za uhalifu watahamasika kutoa taarifa hizo zitakazoiwezesha Serikali kudhibiti na kupambana na uhalifu na kuifanya jamii kuwa sehemu salama ambapo kila mwananchi anatakiwa aishi kwa amani na utulivu, jamii bila uhalifu inawezekana.” Alisema Bi. Makondo.

Bi. Makondo akaziagiza Taasisi za Uchunguzi kuhakikisha taarifa wanazopokea kutoka kwa raia wema zinabaki kuwa siri wakati wote wa uchunguzi. “Tuwatie moyo wananchi, tuwape ushirikiano ili tufikie malengo ya kutungwa kwa sheria hii,” alisema Bi. Makondo.

Akimalizia hotuba yake Bi. Makondo alishukuru programu ya Building Sustainable Anti Corruption Action in Tanzania (BSAAT) kwa kuwezesha kufanyika kwa mafunzo hayo muhimu ya kujenga uwezo wa kutekeleza sheria hiyo na hivyo kuendelea kuimarisha misingi ya utoaji haki kwenye jamii.

Naye Mratibu wa programu ya BSAAT nchini Dkt. Bonaventure Baya akiongea katika mafunzo hayo ameipongeza Wizara kwa uratibu mzuri wa mpango kazi wa kutekeleza programu hiyo na ameahidi kuwa balozi kuitetea Wizara kuendelea kunufaika na programu hiyo ili kuiwezesha kuendeleza mapambano ya uhalifu.

Sheria ya Ulinzi wa Watoa Taarifa na Mashahidi ya mwaka, 2015 na Kanuni zake za mwaka 2023 zina lengo la kuimarisha utawala bora na mapambano dhidi ya uhalifu kwa kuwatambua na kuwalinda watoa taarifa na mashahidi wa makosa hayo wanayoshuhudia yakitendeka katika jamii inayowazunguka.