Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

MAREKEBISHO  YA SHERIA KULINDA MASLAHI YA WANANCHI KUELEKEA DIRA YA TAIFA 2050

Imewekwa: 06 Feb, 2026
MAREKEBISHO  YA SHERIA KULINDA MASLAHI YA WANANCHI KUELEKEA DIRA YA TAIFA 2050

Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Ndg. Eliakim Maswi, amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Nchini, Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Winfrida Korosso, tarehe 05 Februari, 2026 katika ofisi za Wizara Mtumba, Jijini Dodoma.
 
Katika kikao hicho, Mhe. Korosso aliambatana na Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Ndg. George Mandepo, ambapo viongozi hao walijadili kwa kina mchango wa sekta ya Sheria katika kuwezesha na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
 
Mazungumzo hayo yalilenga umuhimu wa kufanya maboresho ya mifumo ya kisheria kupitia utafiti na mapitio ya sheria mbalimbali, ili ziendane na mahitaji ya sasa na ya baadaye ya maendeleo ya Taifa. Maeneo yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na Sheria za Nishati, Sheria zinazohusiana na mabadiliko ya kiteknolojia ikiwemo matumizi ya Akili Bandia (AI), Sheria za Uchumi, Uwekezaji, Biashara (Sura ya 213), Ushirika, Haki Miliki na Haki Shirikishi, Usafiri, pamoja na Sheria za Michezo ya Kubahatisha.
 
Vilevile, kikao hicho kilisisitiza umuhimu wa kuimarisha sekta ya sheria kwa ujumla kupitia utoaji wa elimu ya kisheria kwa wananchi, pamoja na kuandaa mapendekezo ya kisheria yatakayosaidia utekelezaji bora na wenye ufanisi wa sheria nchini.
 
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria aliitaka Tume ya Kurekebisha Sheria kuendelea kutafuta na kupendekeza masuluhisho ya kisheria yatakayosaidia sheria kutekelezeka kwa ufanisi na kuleta tija kwa wananchi.
 
Ikumbukwe kuwa, tarehe 04 Februari, 2026, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, alikutana na uongozi wa Tume ya Kurekebisha Sheria na kuzitaka taasisi za umma kuitumia Tume hiyo kikamilifu katika kufanya tafiti za kina kwenye sheria zenye mapungufu, ili ziweze kufanyiwa marekebisho stahiki.