MASWI AWAPONGEZA WATUMISHI WA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KWA KUTOA HUDUMA BORA NANENANE

Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Eliakim Maswi leo Agosti 10, 2025 ametembelea banda la Wizara hiyo katika maonesho ya Kilimo Nanenane ambayo yamehitimishwa rasmi leo na kuwapongeza watumishi wa Wizara hiyo.
Maswi amewapongeza watumishi wote kwa moyo wa kujitoa na kufanya kazi kwa bidii katika kipindi chote cha siku nane za maonesho na siku mbili zilizo ongezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ambapo wameendelea kuhudumia wananchi mbalimbali waliofika katika banda hilo.
Amesema, "nawapongeza kwa kazi nzuri mliyoifanya tangu siku ya kwanza mpaka leo nimekuta mabanda mengi yamefungwa baada ya tarehe nane lakini ninyi mmendelea kujitoa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, hongereni sana",
Kwa upande wake Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Prosper Kisinini amesema kwa muda wa siku kumi wamehudumia wananchi zaidi ya elfu tano ambao walifika katika banda hilo kupata huduma mbalimbali.
Kisinini amesema wametoa elimu kwa umma kuhusu urai na utawala bora, haki za binadamu, utajiri wa asili na maliasili za nchi pamoja na kushughulikia migogoro ya ardhi, mirathi pamoja na matunzo ya watoto.