MAWAKILI WA KUJITEGEMEA WAHIMIZWA KUHUDUMIA WANANCHI

Mawakili wa kujitegemea Nchini wamehimizwa kujitoa kwa moyo katika kutoa Huduma za Msaada wa Kisheria kwa ufanisi ili kujenga Imani kwa wananchi.
Wito huo umetolewa Septemba 17, 2025 mkoani Morogoro na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Franklin Rwezimula akimuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Ndg. Eliakim Maswi katika ufunguzi wa Mafunzo kwa Mawakili wa Kujitegemea watakao toa Huduma za Msaada wa Kisheria.
Dkt. Rwezimula amewataka mawakili hao kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo kwa kuwa uelewa watakaoupata utawasaidia kuboresha Huduma za Msaada wa Kisheria na kuwa chanzo cha upatikanaji haki kwa wananchi wanaoshindwa kufikia huduma kwa haraka na kupelekea kupoteza haki zao.
Amesema utoaji wa huduma za Msaada wa kisheria ni sehemu ya mchango wao kwa Taifa hivyo basi wanapaswa kuwa waadilifu katika kushughulikia migogoro ya wananchi na kuhakikisha migogoro hiyo inafikia mwisho pamoja na kutoa taaraifa za kila hatua ya kushughulikia migogoro hiyo
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Ester Msambazi alisema kuwa mafunzo haya yanalenga kujadili namna ya kuongeza kasi ya kuwahudumia wananchi wasio na uwezo na wale walio pembezoni ili kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma za mawakili kwa wananchi hao.
"Tutakumbushana pia miiko ya utendaji kazi na wajibu wetu Pamoja na kukubaliana maeneo ya kufanyia kazi ili kuongeza kasi ya kuwahudumia wananchi na kuwa chachu kubwa ya mabadiliko yanayohusiana na masuala ya upatikanaji haki katika jamii'' alisisitiza Msambazi.
Kwa upande wake mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), Rose Nyatega alisema kuwa shirika hilo linashirikiana na wadau na Serikali ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wananchi wote, kuboresha Utawala Bora, Haki za Binadamu pamoja na Usawa wa Kijinsia.