Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Mawakili wa Serikali Simamieni Misingi ya Kazi Zenu - Waziri Kabudi

Imewekwa: 10 Oct, 2024
Mawakili wa Serikali  Simamieni Misingi ya Kazi Zenu - Waziri Kabudi

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi  Oktoba 9, 2024 jijini Dodoma amekutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa  Chama cha Mawakili wa Serikali Nchini.

Akizungumza katika kikao hicho Waziri Kabudi amewataka Mawakili wa Serikali kuhakikisha kuwa wanasimama katika misingi na maadili ya kazi walizoajiriwa nazo Serikalini  kwa  kusimamia haki kwenye utendaji.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Eliakim Maswi amesema kuwa  kwa sasa  Wizara ipo katika mchakato wa kupitia Muundo wa Mawakili ili kuleta umoja, usawa  na kuongeza  ufanisi  katika Kada ya Mawakili wa Serikali nchini.

Bw. Maswi ameweka bayana kuwa Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kushirikiana na Chama hicho katika kutatua changamoto zinazowakabili lakini amesema katika kipindi hiki cha maboresho yanayoendelea rai yake ni kuona matokeo katika utendaji kazi wa Mawakili wa Serikali Nchini.

Awali Makamu wa Rais wa Chama hicho, Wakili wa Serikali Mwandamizi Ellen Rwijage amesema kuwa dhumuni la ziara hiyo ni kujitambulisha kwa Uongozi wa Wizara na kujadili masuala mbalimbali ya Sekta ya Sheria katika Utumishi wa Umma.