Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

MFUMO WA KIDIJITALI WARAHISISHA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA

Imewekwa: 06 Feb, 2026
MFUMO WA KIDIJITALI WARAHISISHA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA

Matumizi ya mifumo ya kidijitali katika  utoaji wa huduma za msaada wa kisheria umeendelea kuwa suluhisho muhimu kwa wananchi kwa kuwezesha upatikanaji wa haki kwa urahisi, haraka na kwa gharama nafuu kupitia Wizara ya Katiba na Sheria.

Akizungumza tarehe 2 Februari, 2026 Mtumba jijini Dodoma, wakati alipotembelea Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Wizara, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema kuwa wananchi wanaweza kupata msaada wa kisheria wakiwa popote walipo bila kulazimika kusafiri kupata huduma kwa kupiga simu Namba 0800004004 au 0262160360.

"Teknolojia inakua kila siku.Sekta ya Sheria nayo hatuna budi kukimbizana na mabadiliko hayo yaliyopo katika kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma.Wananchi wenye uhitaji wa masuala ya kisheria ni wengi sana.Hivyo matumizi ya njia mbadala za mawasiliano kama vile kituo cha huduma kwa mteja ni njia ambayo haiepukiki.Tutangaze ili kila mwananchi afahamu uwepo wa kituo" Alisema Waziri  Homera

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Katiba na Ufuatiliaji wa Haki, Bi. Jane Lyimo,amesema kuwa Wizara imeendelea kuboresha  mifumo ya kidijitali  ili kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi. Bi. Lyimo alieleza kuwa kwa sasa mwananchi ana uwezo wa kupata msaada wa kisheria bila kulazimika kufika kituoni, kwa kutumia njia mbalimbali za mawasiliano ya kidijitali.

“Kwa sasa mwananchi anaweza kupiga simu bure na kuwasiliana moja kwa moja na mtoa huduma kwa ajili ya kutatuliwa changamoto yake. Aidha, anaweza kutuma ujumbe wa WhatsApp kupitia namba 0739 101 910, ujumbe wa kawaida (SMS), au barua pepe (email) malalamiko@sheria.go.tz ili kufikisha shida yake na kupata msaada wa kisheria,” amesema Bi. Lyimo.

Adhma ya Serikali ni kuendelea kuhakikisha kuwa katika mfumo wa upatikanaji haki,wananchi wanafahamu kuhusu haki na wajibu wao, kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika taasisi za utoaji haki, na hivyo kuchangia kujenga imani ya wananchi kwa mifumo ya haki nchini.