Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Mhe. Chana Akutana na Kamati ya Household Committee Kutoka Bunge la Afrika Kusini

Imewekwa: 18 Oct, 2023
Mhe. Chana Akutana na Kamati ya Household Committee Kutoka Bunge la Afrika Kusini

Na George Mwakyembe & William Mabusi - WKS Dododma.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amekutana na wajumbe wa Kamati ya Household Committee on Petitions kutoka Jimbo la Free State Bunge la Afrika Kusini na kufanya nao mazungumzo yanayohusu ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini.

Mhe. Chana amekutana na ujumbe huo tarehe 18 Oktoba, 2023 katika ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma. Katika maongezi hayo Mhe. Chana amesema “Ushirikiano wa Tanzania na Afrika Kusini ni wa kihistoria na wakipee kwani nchi hizi mbili zimekuwa zikishirikiana tangu enzi za kupigania uhuru”.

Aidha, Mhe. Chana ameongeza kuwa “hata sasa ushirikiano baina yetu umeimarika zaidi kwani siyo muda mrefu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan alifanya ziara nchini Afrika Kusini na hii inadhirisha ni namna gani mahusiano yetu yameimarika na kukua zaidi.”

Pia Mhe. Chana amefafanua kuwa biashara baina ya nchi hizi mbili imekuwa ikiimarika kila siku kwani Afrika Kusini wamekuwa wananuzi wakubwa na maparachichi yanayotoka hapa nchini kwetu lakini pia Tanzania imekuwa ikinunua juisi nyingi kutoka Afrika Kusini pamoja na bidhaa nyingine.

Akiongelea umuhimu wa kutumia lugha ya Kiswahili Mhe. Chana amesema “ni wakati mzuri sasa kueneza lugha ya Kiswahili iwe lugha yetu kuu ya mawasiliano kwa nchi zote za Kusini mwa Afrika na pia bara zima la Afrika.

Mhe. Chana ameishukuru Kamati hiyo kwa kuja Tanzania kujifunza mambo mengi, na amewaasa wapate nafasi ya kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo hapa nchini hasa mbuga za wanyama na vivutio vingine.

Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. William Shabalala amesema “Uhusiano baina ya Tanzania na Afrika Kusini hauwezi kusahaulika, na hauwezi kusema chochote kuhusu Uhuru wa Afrika Kusini pasipo kutaja Tanzania maana sisi tuna ndugu Morogoro ambao walipigania Uhuru wakitokea hapa nyumbani Tanzania. Na malengo yetu ya kuja hapa pia ni kujifunza mambo mbalimbali mnayoyafanya maana kwetu Tanzania ni nchi muhimu sana.”

Pia, aliongeza “tunajivunia sana kuwa tupo nyumbani na katika maisha ya sasa ni vyema kizazi chetu kijue kuwa wapi tumetokea na wapi tunaelekea hasa katika mahusino ya nchi hizi mbili, Walichokifanya Waasisi wa Uhuru wetu Mandela na Nyerere ni kitu cha thamani sana ambacho kimetufanya tuwe pamoja mpaka sasa.”