Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Mhe. Gekul Aongoza Kikao cha Kujadili Mpango Kazi wa Taifa wa Haki za Binadamu na Biashara

Imewekwa: 26 Aug, 2023
Mhe. Gekul Aongoza Kikao cha Kujadili Mpango Kazi wa Taifa wa Haki za Binadamu na Biashara

Na George Mwakyembe, Emmanuel Msenga na Faraja Mhise - WKS

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul (MB) ameongoza kikao cha kujadili mpango kazi  wa Taifa  wa Haki za Binadamu na Biashara (National Action Plan on Business and Human Right in Tanzania Mainland and  Zanzibar) kilicholenga kuangazia masuala ya Haki za Binadamu  hasa kwenye nyanja ya biashara  kama vile uwekezaji  pamoja na shughuli zingine za kibiashara huku ukizingatia masaula ya haki za binadamu wakati wa utekelezaji wake.  

Kikao hicho ambacho kimehusisha Wizara na Taasisi mbalimbali kimefanyika tarehe 25 Agosti 2023 katika ukumbi wa Morena Jijini Dodoma. 

Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi ameipongeza Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kushirikiana vyema na Wizara mbalimbali, Idara za Serikali, Taasisi za Umma, Sekta binafsi, Asasi za kiraia, pamoja na wafanyabiashara na Wadau wa Maendeleo ya jamii kwa ujumla. 

Mhe. Gekul ameongeza kuwa kufanyika kwa kikao hicho ni moja ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kupitia Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kushirikisha wadau mbalimbali katika mchakato wa kuandaa mpango wa kitaifa wa Haki za Binadamu na biashara pamoja uwekezaji.

Aidha, Mhe Gekul ameitaja Tanzania kuwa ni moja kati ya nchi kumi zilizoanzisha mpango huo kati ya nchi hamsini na nne za Afrika. 

Wakati huo huo Gekul ameipongeza Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kupata hadhi ya daraja ‘A’, ya Mtandao wa Taasisi za Kimataifa za Haki za Binadamu ulimwenguni.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Bw. Mohamed Khamis Hamad akigusia umuhimu wa masuala ya haki za binadamu katika uwekezaji amesema, “ni vyema uwekezaji ukazingatia Haki za Binadamu na kuzilinda, tayari nchi za Kenya na Uganda walisha andaa mpango kazi kama huu ili kuondoa manyanyaso na ukiukwaji haki na sasa wapo kwenye utekelezaji.”

Akiongea kwenye kikao hicho, Mshauri wa masuala ya utawala bora kutoka shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa Bw. Godfrey Mulisa amesema Haki za Binadamu na biashara ni uwanja mpana utakaowasaidia wafanyabiashara  katika ufanyaji wa biashara zao huku wakizingatia haki za Binadamu. 

Pia ameahidi kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kushirikiana na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora katika utakelezaji wa mpango kazi huo.

Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Bw. Patience Ntwina ameishukuru Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano wanaowapa katika kutekeleza suala zima la Haki za Binadamu. Pia Bw. Ntwina ameongeza kuwa mchakato wa kuandaa mpango kazi wa Haki za Binadamu na biashara  umetokana na andiko ambalo liliwasilishwa katika Wizara ya Katiba na Sheria baada ya kufanyika vikao kadhaa ambapo walipendekeza kuwepo na majadiliano ambayo yatawahusisha wadau mbalimbali ili kufanikisha mpango kazi huo hivyo maoni na mapendekezo ya kikao hicho yatawezesha kuboresha mpango kazi huo  kwa maendeleo endelevu ya Taifa.

Kikao hicho kimeandaliwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG) kwa kushirikiana na Shirika la Maenedeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa lengo la kuwajengea uelewa wa kuzingatia masauala ya Haki za Binadamu wakati wa utekelezaji wa biashara na uwekezaji.