Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Mhe. Gekul Awasilisha Sheria Ndogo Kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge

Imewekwa: 24 Aug, 2023
Mhe. Gekul Awasilisha Sheria Ndogo Kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul amewasilisha sheria ndogo ya kumlinda mtoa taarifa pamoja na mashahidi (The WhistleBlower and Witness Protection Act Cap. 446), katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo. Akiwasilisha mbele ya Kamati Mhe. Gekul ameiambia Kamati kuwa sheria hiyo ni muhimu na itasaidia katika kumlinda mtoa taarifa pamoja na ushahidi na kumpa mwongozo wa kudai haki zake  mara tu baada ya ushahidi kukamilika.

Mhe. Gekul amewasilisha Sheria hiyo tarehe 24 Agosti, 2023 kwenye ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma na kuwataka wajumbe watoe maoni pamoja mapendekezo ili kuweza kuboresha zaidi.

Kikao hicho ambacho kimeongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo Mhe. Ramadhan Suleiman Ramadhan (MB), ametoa mapendekezo ya kuwa katika sheria hiyo kuwepo na muundo mmoja wa uandishi wa barua ambao utatumika kujibu barua ya mwombaji wa ulinzi ili kuepusha utofauti katika kujibu maombi hayo.

Vile vile kamati imependekeza kuwa muda wa Waziri kufanya maamuzi juu ya rufaa ya mwombaji wa ulinzi iwe ni siku 21 tu na si ndani ya siku 30 kama inavyoonesha sasa. Hivyo kamati imetaka Waziri pamoja na watalaam kufanya marekebisho katika vifungu hivyo.

Aidha, Kamati imependekeza kuwa mwombaji apewe taarifa ya kukubaliwa au kukataliwa ombi la kulindwa kwa ndani ya siku 14 na iwapo mwombaji hataridhika basi anaweza kukata rufaa  kwa Waziri wa Katiba na Sheria.

Naibu Waziri Gekul ameishukuru Kamati kwa mapendekezo pamoja na maoni waliyotoa na kuahidi kufanyiwa kazi na kuleta sheria hiyo ambayo itakuwa imezingatia maboresho  na maoni yote waliyopendekeza.