Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Mhe. Gekul: Fanyeni tafiti maeneo yanayoongoza katika ukiukwaji wa haki za Binadamu

Imewekwa: 23 Mar, 2023
Mhe. Gekul: Fanyeni tafiti maeneo yanayoongoza katika ukiukwaji wa haki za Binadamu

Na William Mabusi – WKS

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul (Mb) ameiagiza Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kufanya utafiti na kubaini maeneo yanayoongoza katika masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu ili iweze kuishauri Serikali maeneo ya kipaumbele katika kuelekeza nguvu za kukabiriana na ukatili na matukio mengine yanayokiuka haki za kibinadamu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji kwa vitendo nia ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kupambana na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Mhe. Gekul alitoa kauli hiyo alipokutana na kufanya mazungumzo na sehemu ya Menejimenti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyofika ofisini kwake Makao Makuu ya Wizara ya Katiba na Sheria, Mtumba – Dodoma, tarehe 22/03/2023 kwa lengo la kujitambulisha rasmi kwake na kumpitisha katika majukumu ya Tume hiyo.

Moja kati ya maeneo ambayo katika mazungumzo hayo Mhe. Gekul alijengewa ufahamu na Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Bw. Patience Ntwina ni pamoja mamlaka iliyonayo Tume ya kufanya uchunguzi pale inapobainika kuwepo kwa uvunjifu wa Haki za Binadamu; Kupitia sheria za ndani kuona kuwa zinakidhi msingi ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na kushauri Serikali kuhusu Mikataba ya Kimataifa na Kikanda katika kuboresha haki za binadamu.

 “Fanyieni utafiti maeneo ya Mikoa inayoongoza kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, vitendo vya uuaji, ubakaji na ulawiti.” Aliagiza Mhe. Gekul

Mhe. Naibu Waziri ameitaka Tume kuchagua haki kadhaa na kuzipa kipaumbele cha kuzifanyia tafiti kulingana na bajeti wanayopewa. Taarifa za tafiti hizo zitolewe kwa mamlaka husika kwa ajili ya utekelezaji, kitu ambacho kitapelekea kazi zinazofanywa na Tume kujulikana zaidi kwa wananchi na wadau wengine wa haki za binadamu.

Aidha, Mhe. Gekul ameshauri kuwepo na ushirikiano wa kutumia majengo ya Serikali, akitolea mfano majengo ya Vituo Jumuishi vya utoaji haki ili kuwezesha watumishi wengi wa Tume kufanya kazi mikoani. Kikao hicho kimefanyika ikiwa ni mwendelezo wa kazi aliyoanza kuifanya ya kutembelea na kujifunza utendaji na majukumu ya Taasisi zilizo chini ya Wizara toka alipoteuliwa na Mhe. Rais kuwa Naibu Waziri Katiba na Sheria Februari mwaka huu.