Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

ULEGA ATILIA MKAZO MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA KWA WATOTO

Imewekwa: 16 Oct, 2026
ULEGA ATILIA MKAZO MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA KWA WATOTO

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa watoto kupitia ushirikiano wa taasisi za Serikali na wadau mbalimbali, ili kuhakikisha watoto wanalindwa na kupata haki stahiki.

Mhe. Ulega ameyasema hayo  tarehe 13 Oktoba, 2026 katika ziara yake ya kujitambulisha ambapo amekutana  na Menejimenti na Watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka katika ofisi za taasisi hiyo zilizopo Njedengwa, jijini Dodoma.

Katika ziara hiyo Waziri Ulega amepokea  taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya ofisi hiyo na kujadili mipango ya kuimarisha huduma za kimashtaka nchini.

Amesema ni muhimu kuimarisha juhudi za kuanzisha kituo maalumu cha kushughulikia mashauri ya ukatili dhidi ya watoto, akieleza kuwa hatua hiyo inahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na wadau wengine.

“Nitalibebea bango suala hili. Nitaenda kukaa na wenzangu ili kuweka msukumo wa pamoja kuhakikisha jambo hili linatimia,” amesema Mhe. Ulega.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kufanya tafiti ili kubaini sababu na viashiria vinavyochangia vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, akieleza kuwa vitendo hivyo vinaweza kusababisha madhara ya kisaikolojia yanayoendelea kuathiri maisha ya waathirika hadi wanapokuwa watu wazima.

Awali, Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini, Bw. Sylvester Mwakitalu, amesema idadi ya watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeongezeka kutoka 630 mwezi Machi 2021 hadi kufikia 1,264, hatua iliyochangia kupanua huduma za kimashtaka nchini.

Aidha, amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, kupitia Wizara ya Katiba na Sheria, imewasilisha maombi kwa Tume ya Mipango kuhusu mradi ya miaka mitano inayolenga kuimarisha mifumo ya kushughulikia uhalifu wa kifedha.