LST IWAANDAE MAWAKILI WENYE UBORA- WAZIRI ULEGA
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega, ameitaka Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST), kuzingatia ubora wa mafunzo yanayotolewa ili kuwaandaa Mawakili wenye weledi, uwajibikaji na viwango vya juu vya kitaaluma vinavyoendana na mahitaji ya Watanzania.
Waziri Ulega ametoa rai hiyo leo, Oktoba 15, 2026, alipokutana na Viongozi na Menejimenti ya Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa lengo la kujitambulisha na kufahamu majukumu, utendaji na mipango ya Taasisi hizo tangu alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Ulega amesema LST ina nafasi muhimu katika mfumo wa utoaji haki nchini kwa kuwa ni Taasisi inayowaandaa Wanasheria kabla ya kuingia katika taaluma ya Uwakili, hivyo inapaswa kuhakikisha mafunzo yake yanakidhi viwango vinavyotarajiwa na jamii.
“Nimefahamishwa kuwa Taasisi hii ndiyo chujio la mwisho katika kuwapika Wanasheria kwenda kufanya kazi za Uwakili. Kwa kulifahamu hili na kujua umuhimu wa mafunzo yanayotolewa na Taasisi hii, naomba niwasihi sana Watumishi wenzangu na Viongozi kuhakikisha kuwa mafunzo mnayoyatoa yanazingatia ubora unaotegemewa na Watanzania na walaji kwa ujumla.”Amesema Waziri Ulega.
Amesisitiza kuwa ubora wa mafunzo hayo unapaswa kuambatana na weledi na uwajibikaji ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia viwango vya kitaaluma na mahitaji ya wakati uliopo.
“Ni muhimu kuzingatia weledi, uwajibikaji na kuhakikisha mnatoa Wanasheria wenye viwango vya juu vya ubora vinavyoendana na wakati tulionao.”Amesisitiza Waziri Ulega
Waziri Ulega ameongeza kuwa kuwaandaa Mawakili wasio na uwezo wa kutosha kunaweza kusababisha hasara kwa wateja wanaowahudumia na Taifa kwa ujumla. Ameeleza kuwa taaluma ya Sheria ni muhimu katika ustawi wa nchi kwa kuwa inatoa ushauri wa kisheria na miongozo inayosaidia taasisi na watumishi kutekeleza majukumu yao kwa usahihi na kwa kuzingatia sheria.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Balozi Baraka Haran Luvanda amesema Wizara itaendelea kushirikiana na Taasisi hiyo ili kuiwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa LST, Mkuu wa Taasisi hiyo, Profesa Sisty Mramba, amesema kuwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007, jumla ya Mawakili 11,217, sawa na asilimia 59 kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa, wamehitimu mafunzo na kuapishwa kuwa Mawakili, hatua ambayo imeongeza tija katika mnyororo wa utoaji haki nchini.