ULEGA AWAASA WANAFUNZI LST KUTUMIA TEKNOLOJIA KWA TIJA
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega, amewataka wanafunzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST) kutumia maendeleo ya teknolojia, ikiwemo Akili Unde (AI), kwa manufaa yao binafsi, jamii na Taifa kwa ujumla.
Waziri Ulega ametoa wito huo leo, Oktoba 15, 2026, wakati akizungumza na wanafunzi wa kundi la 43 katika Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa lengo la kujitambulisha na kufahamu majukumu, shughuli na mipango ya Taasisi hizo tangu alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Waziri Ulega amewahimiza wanafunzi hao kutumia muda wao wa mafunzo kwa bidii, kujenga weledi na kuhakikisha wanapata maarifa na ujuzi utakaowawezesha kutekeleza majukumu yao ya kisheria kwa ufanisi baada ya kuhitimu.
Amesema matumizi sahihi ya teknolojia ni muhimu katika kuboresha ubora wa mafunzo na kuwawezesha wanafunzi kuendana na mabadiliko yanayotokea katika sekta ya sheria na dunia kwa ujumla.
“Itumieni teknolojia vyema kupata ubora wa kile mlichokifuata hapa. Hakikisheni mnafanya kwa bidii na juhudi zenu zote. Msipoteze wakati wenu hapa; hapa pawe mahali ambapo ukitoka utasema nilipata maarifa na ujuzi katika Law School of Tanzania,” amesema Ulega.
Ameongeza kuwa wanafunzi wanapaswa kuhakikisha elimu wanayoipata inawanufaisha wao wenyewe, jamii na Taifa, huku wakizingatia maadili na weledi katika matumizi ya teknolojia.
“Dunia imeenda kwenye mabadiliko ya kiteknolojia, ikiwemo mabadiliko ya Akili Unde (AI). Ninyi mawakili wasomi, itumieni kama faida kwenu na si kuitumia vibaya,” amesisitiza Waziri Ulega.
Aidha, Waziri Ulega ameeleza kuwa taaluma ya sheria ina fursa mbalimbali za kushiriki katika shughuli za ujenzi wa Taifa, hivyo mafanikio ya kila mwanafunzi yatategemea kwa kiasi kikubwa malengo aliyojiwekea, juhudi zake na namna anavyotumia maarifa anayopata katika mafunzo yake.
Amesema Serikali inaendelea kuhimiza matumizi ya teknolojia katika kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza ufanisi katika taasisi mbalimbali, ikiwemo zile zinazotoa mafunzo na huduma za kisheria.
Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo, Profesa Sisti Mramba, amesema taasisi hiyo imeendelea kutumia mbinu mbalimbali za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kuboresha mafunzo na usimamizi wa wanafunzi.