Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

WIZARA, WADAU WAKUTANA KUJADILI CSV KUELEKEA DIRA 2050

Imewekwa: 23 Sep, 2026
WIZARA, WADAU WAKUTANA KUJADILI CSV KUELEKEA DIRA 2050

Wizara ya Katiba na Sheria, kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu, imewakutanisha wadau kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali kujadili namna Mfumo wa Thamani ya Pamoja (Creating Shared Value – CSV) unavyoweza kutumika kama nyenzo ya kimkakati katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akifungua kikao hicho Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Uangalizi wa  Utajiri Asili na Maliasilia za Nchi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Evarist Mashiba, leo Septemba 22, 2026 katika ukumbi wa wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma amesema majadiliano hayo ni muhimu katika kuhakikisha kuwa shughuli za biashara na uwekezaji katika mali na rasilimali asilia zinaendelea kuleta manufaa kwa wadau mbalimbali na kuchangia maendeleo ya wananchi pamoja na Taifa kwa ujumla.

Mashiba ameleza kuwa mjadala huo ulilenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu dhana ya CSV na namna inavyoweza kutambuliwa katika sera, sheria au miongozo ya uwekezaji, ili kuwawezesha wazawa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi zinazotokana na uwekezaji na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za uchumi.

“Dhamira ni kuhakikisha uwekezaji wa leo unajenga uwezo na shughuli za kiuchumi zitakazoendelea kuzalisha ajira, kipato na manufaa kwa Taifa na wananchi hata baada ya uwekezaji husika kufikia ukomo” amesema Mashiba.

Majadiliano hayo yanaweka msisitizo wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 unaolenga kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani kupitia sekta imara ya biashara inayojumuisha biashara ndogo, za kati na kubwa, zinazomilikiwa na wafanyabiashara wa ndani na wa kigeni pamoja na mashirika ya umma ya kibiashara. 

Majadiliano hayo na wadau yana umuhimu katika kuweka mazingira ya kisheria yanayowezesha biashara na uwekezaji, sambamba na kuhakikisha sheria na mifumo ya haki inaendana na mahitaji ya uchumi wa kisasa na malengo ya Dira 2050.